Klabu zataka Ligi Kuu, FA zifutwe

Friday April 3 2020

 

By Imani Makongoro, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku 17 kumalizika kwa siku 30 ambazo Serikali ilitangaza kusitisha mikusanyiko ikiwamo shughuli za michezo, klabu mbalimbali za Ligi Kuu zimesema kuna haja ya ligi kufutwa msimu huu.

Klabu hizo zimekwenda mbali na kutaka matokeo ya msimu uliopita ndiyo yatumike kuamua bingwa na timu zilizo kwenye hatari ya kushuka daraja kutafutiwa njia mbadala.

Ligi Kuu ni sehemu ya matukio yaliyosimama kipindi hiki cha tahadhari ya ugonjwa wa corona unaotikisa dunia.

Licha ya jana, taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kueleza kwamba kuna uwezekano msimu kwenda hadi mwishoni mwa Juni, lakini kama janga la corona litaendelea, vyombo vinavyosimamia ligi vitafanya uamuzi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo alisema jana kuwa maazimio waliyofikia awali kuhusu mwenendo wa Ligi Kuu yako palepale na hakuna kilichobadilika.

Maazimio hayo ni ligi kufikia tamati Juni, wachezaji kupimwa maambukizi ya corona kabla ya mechi endapo Serikali itaruhusu mechi kuchezwa bila mashabiki.

Advertisement

Licha ya mkakati huo, viongozi wa klabu za Ligi Kuu wamesema kwa namna hali ilivyo, hawatarajii kama baada ya Aprili 17 ligi itaendelea na kuishauri TFF kuifulicha ya kufikia mzunguko wa 29.

Simba ndiyo inayoongoza ikiwa na pointi 71, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 54, zote zimebakisha mechi 10. Yanga ni ya tatu ikiwa na pointi 51 na michezo 11 mkononi.

Singida United ni ya mwisho ikiwa na pointi 15, ikifuatiwa na Mbao (22), Alliance (29), Mbeya City (30), Ndanda (31), KMC, Mtibwa Sugar na Lipuli zenye pointi 33 kila moja na mechi tisa mkononi.

Msimu huu timu nne zinapaswa kushuka daraja na mbili kucheza playoff kutafuta tiketi ya kubaki, lakini pia kanuni zinasema bingwa anapaswa kucheza mechi zake zote na kumaliza.

Makamu mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alisema pamoja na matarajio ya TFF hawatarajii kama kama hali itakuwa salama. “Naona TFF ingetumia msimamo wa msimu uliopita tu kuamua bingwa, aliyekuwa bingwa msimu uliopita apewe ubingwa wa msimu huu na hapa tulipofikia msimu huu basi Ligi iahirishwe tuanze upya msimu ujao, bila shaka janga hili litakuwa limepita na timu zimejipanga” alisema.

Alisema timu ambazo ziko katika hatari ya kushuka daraja zitafutiwe utaratibu wa kushindanishwa ili kupata ambazo zitashuka, lakini hakuna uhakika kwamba kufikia Juni hali itakuwa salama.

Kauli ya Mwakalebela imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Lipuli, Benedict Kihwelu ambaye alisema, “TFF ingetumia busara kuahirisha Ligi, kwani hata ikifanyika, morali ya wachezaji haitokuwepo, bado kuna hamaki juu ya hili janga ambalo hatujui kipindi hicho TFF walichosema litakuwa liko kwenye hatua gani?

“Kilichopo ni bingwa apatikane lakini kwa kuangalia rekodi yake katika msimamo na nafasi ya wale walio nyuma yake kutwaa ubingwa ikoje? na walio kwenye hatari ya kushuka nao waangaliwe wameachana pointi ngapi?”

Alisema hata kombe la Shirikisho (FA) linapaswa kufutwa na bingwa wa msimu uliopita aendelee.

Katibu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema TFF iangalie mashirikisho mengine ya soka duniani yanafanya nini kipindi hiki, ingawa naye ameshauri ligi ifutwe na kuanza upya.

“Matokeo ya msimu uliopita yaendelee msimu huu, ingawa hilo linahitaji uamuzi wa pamoja wa klabu,” alisema Kimbe.

Kocha wa Mbao, Abdul Mutiki Hajji alisema TFF ikiweza isimamishe ligi na kutafuta njia mbadala ya kupata bingwa wa msimu huu na timu za kushuka daraja.

Kaimu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Mwina Kaduguda alisema ni mapema kulizungumzia hilo.

Mchambuzi wa soka na aliyewahi kuwa nahodha wa Yanga, Ally Mayay alisema yanahitajika makubaliano ya kitaifa ya wadau wa soka kuhusu hatima ya ligi.

“Afya ni kitu kingine na michezo ni kitu kingine, kwa hali ilivyo katika suala la corona kunahitaji zaidi makubaliano ya kitaifa ili kujilinda na janga hilo,” alisema Mayay.

Advertisement