Mafundi 7 wa namba 7 mgongoni

Tuesday September 10 2019

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Miongoni mwa namba za jezi ambazo zimekuwa zikivaliwa na nyota kadhaa ambao wamekuwa wakifanya vizuri, huwezi kusita kuzitaja namba 7 na 10 ambazo kwa kizazi hiki wametamba nazo, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Wanasoka hao ni washindi wa tuzo za Mchezaji Bora wa Dunia (Ballon d’Or) mara tano kila mmoja, wamekuwa kwenye viwango bora kwa zaidi ya misimu 10 ya uchezaji wao wa soka la ushindani.

Mbali na jezi namba 10, tujikite kwenye namba saba kwa kuangalia wachezaji ambao wameiletea heshima namba hiyo kwenye klabu zao, akiwemo Ronaldo tangu akiwa Manchester United ya England hadi alipotua Real Madrid ya Hispania na sasa Juventus.

Jadon Sancho

Jadon Sancho wa Borussia Dortmund ni kati ya makinda yanayofanya vizuri. Msimu uliopita alikuwa mchezaji mwenye umri mdogo kwenye Ligi ya Ujerumani kufikisha mabao 15, alivunja rekodi iliyodumu kwa miaka 52.

Jose Callejon

Advertisement

Winga wa Napoli, Jose Callejon ni moto wa kuotea mbali, ameifanya timu hiyo ya Italia kuwa na makali kwenye maeneo ya pembeni, alianza kung’ara chini ya Maurizio Sarri .

Amekuwa mchezaji muhimu wa Gli Azzurri tangu 2013 akitokea Real Madrid huku akifunga mabao 79 na kutengeneza mengine 69 akiwa nchini Italia.

Son Heung-min

Tottenham Hotspur sio klabu ambayo kwenye uchezaji wake imekuwa ikitegemea mawinga tangu kuondoka kwa Gareth Bale. Lakini uwepo wa Mkorea Kusini, Son Heung-min, umewafanya kuwa na nguvu kwenye maeneo hayo licha ya kuwa na uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa kati.

Idadi ya mabao 60 aliyofunga ndani ya msimu mitatu akiwa na Tottenham, Son amekuwa moja ya wachezaji hatari England wenye uwezo wa kucheza maeneo tofauti ya ushambuliaji.

Msimu uliopita aliifungia Tottenham mabao 20 na kutengeneza mengine 10 kwenye mashindano yote.

N’Golo Kante

N’Golo Kante alikuwa sehemu ya mafanikio ya Leicester City ile iliyofanya maajabu kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2015/16, alipotua tu Chelsea msimu uliofuata alibeba tena ubingwa huo.

Amekuwa akicheza eneo la kati la kiungo pamoja na kuwa muda mwingine alikuwa akichezeshwa kama winga anayekaa eneo la kati zaidi chini ya Maurizio Sarri ambaye kwa sasa anaifundisha Juventus ya Italia.

Raheem Sterling

Manchester City wanaye mmoja wa washambuliaji hatari katika Ligi Kuu England kama sio Ulaya, ameonyesha hilo akiwa na Pep Guardiola ndani ya msimu miwili iliyopita, si mwingine bali ni Raheem Sterling.

Akiwa na jezi namba saba mgongoni amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Guardiola ambapo msimu uliopita alifunga mabao 17 huku akitengeneza mengine 10.

Kylian Mbappe

Hakuna mchezaji maarufu zaidi ya Kylian Mbappe wa Paris Saint-Germain kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 barani Ulaya. Akiwa na umri mdogo nyota huyo alifanya makubwa kwenye Kombe la Dunia lililopita nchini Russua akiwa na Ufaransa.

Mchezaji huyo wa zamani wa Monaco angetwaa msimu uliopita ufungaji bora wa Ulaya akiwa na mabao 33 kama sio uwepo wa Messi ambaye aliibuka kuwa mfungaji bora kwa mara ya sita akiwa na mabao 36.

Cristiano Ronaldo

Hakuna shaka kwamba Cristiano Ronaldo ndiye mchezaji bora zaidi anayevalia jezi namba saba licha ya msimu uliopita akiwa na Juventus alishindwa kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Italia.

Pamoja na kushindwa kuwa mfungaji bora, Ronaldo aliisaidia Juventus kutwaa ubingwa wa ligi hiyo ambayo ni marufu kama Serie A huku akiibuka kuwa MVP wa msimu huo nchini humo.

Majeraha ya Eden Hazard ambaye atavaa jezi namba saba msimu huu Real Madrid yamemfanya asianze kuitumikia jezi yake hiyo mpya mgongoni. Klabu ya kutua Madrid, Hazard alivaa jezi Na.10 Chelsea.

Advertisement