Malima amtaka Gadiel aondoke Simba

Dar es Salaam. Mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ amemshauri beki wa Simba, Gadiel Micheal kuangalia uwezekano wa kuhamia timu nyingine katika msimu unaokuja.

Malima alisema jana kwamba Gadiel ana kipaji na ili akiokoe, anatakiwa kuondoka Simba alikoshindwa kutamba mbele ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye anaaminiwa kwenye kikosi cha kwanza.

“Sina maana mbaya kumshauri hivyo kwa sababu ni muda wake wa kucheza, hivyo lazima abadili upepo anapoona haoni mwelekeo wa yeye kucheza,” alisema.

Alisema Gadiel ni miongoni mwa wachezaji vijana ambao wanapaswa kuitumikia timu ya taifa akiwa kwenye ushindani na kiwango cha juu, akisisitiza kwamba kukaa kwake benchi hakumpi taswira nzuri.

Ukiachana na Gadiel, Malima alimtaja beki wa Namungo FC, Hamis Mgunya kwamba anapaswa kutupiwa jicho akiamini atafanya maajabu Stars.

“Lazima tukubali kwamba umri wa Kelvin Yondani na Erasto Nyoni unaelekea jioni na ni wachezaji muhimili kwenye kikosi cha Stars, lazima waandaliwe vijana mahiri.”

Alisema mbali ya kuitwa Stars, Malima alisema pia Simba na Yanga zinaposajili zinatakiwa kuangalia vipaji kutoka timu za ndani.

“Sio kwamba napinga wachezaji wa kigeni, ila kuna wazawa ambao wana uwezo wa juu ambao unaweza kuwa msaada Stars.”