Mapema tu, Kaze yuko Uwanjani

Wednesday October 21 2020
kaze pic

YANGA imewatoa hofu mashabiki kwa kuthibitisha kesho Alhamisi kwa mara ya kwanza Kocha wao mpya, Cedrick Kaze atakuwa kwenye benchi kuiongoza timu hiyo dhidi ya Polisi Tanzania.

Mechi hiyo ya Ligi itapigwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru ambao una nyasi bandia.

Kaze ambaye ana uzoefu na soka la Cecafa, amesaini mkataba wa miaka miwili Ijumaa iliyopita kuifundisha timu hiyo akitokea Canada.

Yanga mapema Ijumaa ilianza mchakato huo ili kocha huyo aweze kufanya kazi yake kwa uhuru licha ya kwamba anabebwa pia na kutokea ukanda wa Afrika Mashariki ambao unamruhusu kufanya kazi kwa miezi mitatu wakati michakato mingine ikiendelea.

Ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alikiri ni kweli walishalipia kibali hicho na wamejiridhisha ataendelea na majukumu yake kama kawaida akisaidiana na Juma Mwambusi na Vladmir Niyonkuru.

“Kwa mujibu wa mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanachama wake wote wanaweza kuingia na kufanya kazi kwa kipindi cha miezi mitatu, pia wanaweza kuingia kuishi na kufanya shughuli za kwa kipindi cha miezi sita, sisi tulishalipia kila kitu, Alhamisi atakuwepo katika benchi,” alisema.

Advertisement

Kaze aliliambia Mwanaspoti anashukuru kwa kuanza kazi yake vizuri na amepata ushirikiano mkubwa kwani tayari alikuwa akiwajua wachezaji kabla hajatua kambini na wengi wao alishazungumza nao na kukiri kuhusika na usajili wa wachezaji wa kigeni wa Yanga kabla hajatua Jangwani msimu huu.

Kaze mpaka sasa katika mazoezi yake amekuwa akitoa msisitizo kwa wachezaji wake kucheza mpira wa haraka haraka kuelekea katika lango la wapinzani ili kupata bao la mapema.

Anaamini kwa kucheza mpira huo unakuwa unajilinda lakini pia unawapa nafasi ngumu wapinzani kufanya vizuri, badala yake unatumia makosa yao kuhakikisha unafunga.

Advertisement