Mgawo wa Samatta ukweli ni huu hapa

Sunday January 19 2020

 

By Thomas Ng’itu, Mwananchi tng’[email protected]

Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amefafanua kuhusu mgawo wa pesa ambao klabu hiyo ya Msimbazi itapata kutokana na mauzo ya straika wao wa zamani Mbwana Samatta kutoka katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji kwenda Aston Villa ya Ligi Kuu ya England.

Awali, aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage alikaririwa katika moja ya kituo cha radio akisema kwamba Simba itaendelea kupata mgao wa asilimia 20 kwa kila timu ambayo mchezaji huyo atauzwa.

Hata hivyo, Senzo ameweka sawa jambo hilo akisema mkataba wa asilimia 20 ya pesa ya uhamisho wa Samatta halipo tena kwani liliishia katika mkataba wa Simba na TP Mazembe pale straika huyo aliposajiliwa na Genk.

“Hapana hilo suala kwa muda huu halipo kwasababu mkataba ulikuwa ni kati ya Simba na Mazembe, Samatta angeuzwa popote pale na Mazembe basi Simba walikuwa wanapata asilimia 20 na ilikuwa hivyo, lakini iliishia tu pale alipoenda Genk,” alisema.

Aliongeza kuhusu uhamisho wa Samatta kutoka Genk kwenda Aston Villa, klabu hiyo ya Msimbazi haitapata mgao wowote ule nje ya mgao maalumu wa kanuni ya FIFA (solidarity).

“Hakuna mkataba unaotaka Genk waipe pesa Simba kupitia Samatta, lakini kinachosubiriwa muda huu ni kujua pesa ambayo tutaipata kupitia uhamisho wake kwahiyo ikitoka tutajua kupitia mgao ambao utakuwapo na sio Simba peke yake bali timu zote ambazo amepita,” alisema.

Advertisement

Mgao ambao utatoka katika pesa ya usajili wa Samatta ni asilimia 5 inayogawanywa kwa timu zote zilizomgharamia mafunzo na elimu akiwa chini ya miaka 23 kabla hajasaini mkataba wa kwanza wa kucheza soka la kulipwa Ulaya.

Kwa maana hiyo asilimia 5 ambayo itapatikana katika mauzo hayo, itagawanywa kwa klabu za Africa Lyon, Simba na TP Mazembe.

FURAHA YATAWALA

Adi Yussuf ambaye anaichezea Boreham Wood kwa mkopo akitokea Blackpool ya Daraja la Pili England, anasema wataendeleza kwa pamoja usemi wao wa ‘haina kufeli’ ambaowamekuwa wakipenda kuutumia.

“Nimefurahishwa na ujio wake. Atafurahia maisha ya England na ushindani wa ligi, niliwahi kumshawishi na kutaniana naye kuwa umefika muda wa kuja England, alikuwa akicheka na kusema tusubiri muda sahihi,” alisema Adi.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ammy Ninje ambaye kwa sasa yupo England, anasema Samatta ana ubora wa kumudu mikiki ya Ligi Kuu nchini humo. “Alionyesha katika mchezo dhidi ya Liverpool tena katika mashindano makubwa ya Ligi ya Mabingwa, namwona kama mkombozi wa Aston Villa, anaweza kuchangia kwa timu hiyoisishuke daraja,” anasema Ninje mwenye taaluma ya ukocha.

Saimon Msuva ambaye anaichezea Difaa El Jadida ya Ligi Kuu Morocco, alisema Samatta ameendelea kuwa mfano hai kwao hivyo kutua kwake England ni ishara tosha kuwa kwa sasa milango imefunguka rasmi kwa Watanzania kucheza ligi hiyo kubwa duniani.

“Tangu tukiwa wadogo tumekuwa wafuatiliaji wazuri wa EPL. Kupata nafasi ya kucheza ligi hiyo sio jambo jepesi, anastahili pongezi kwakweli Samatta na naamini huo ni mwanzo kuna kundi jingine la wachezaji kutoka Tanzania linakuja,” alisema Msuva.

Msuva ambaye hivi karibuni alikuwa akihusishwa kujiunga na Benfica ya Ureno, anaongeza kwa kusema, “Sina shaka na uwezo wa Samatta, haitokuwa ajabu akiendelea kufanya vizuriakiwa nchini humo kama ilivyokuwa Ubelgiji.”

Advertisement