Ndayiragije aifungia kazi Guinea ya Ikweta

Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku 18 kabla ya Taifa Stars kupepetana na Guinea ya Ikweta katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Afrika (Afcon) 2021, Kaimu Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije amesema wapinzani wao ni timu tishio.

Mchezo huo kwanza kwa Taifa Stars katika Kundi J utachezwa Novemba 10 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kabla ya kwenda ugenini kuivaa Libya katika mechi itakayochezwa wiki moja baadaye.

Ndayiragije aliliambia gazeti hili jana kuwa, Guinea ya Ikweta sio timu ya kubeza katika kundi lao na anaiweka kwenye daraja moja na Tunisia, Libya.

“Guinea ya Ikweta inaonekana timu ya kawaida katika kundi letu, lakini kama watu wataifuatilia vizuri watakubaliana na mimi tusipojiandaa vizuri wanaweza kutusumbua kwenye mechi ambayo tutacheza nao,” alisema.

“Guinea ina kikosi kinachoundwa na kundi la wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi yao na wana ubora wa hali ya juu. Tisa wamezaliwa na kukulia Ulaya nchini Hispania ambako wamelelewa kwenye vituo vya soka vya klabu za Barcelona, Santander, Malaga na Atletico Madrid.”

“Bado kuna wengine ambao wenyewe walienda Ulaya wakiwa na umri mdogo na wamecheza huko kwa muda mrefu, hivyo wana ubora na uzoefu wa kutosha wa kucheza mechi za mashindano makubwa na magumu kama haya ya kuwania kufuzu.”

Wachezaji tisa wa kikosi cha Guinea ya Ikweta waliozaliwa na kukulia Hispania kwenye vituo vya klabu za Ulaya ni Emilio Nsue, Aitor Embela, Igor Engonga, Luis Meseguer, Esteban Obiang, Ruben Belima, Paulo Ganet, Niko Kata na Jannick Buyla.

Nahodha wa Guinea ya Ikweta, Emiliano Nsue (30) anayecheza Apollon Limassol ya Cyprus, alizaliwa na kukulia kituo cha Mallorca, Hispania. Pia alicheza Mallorca, Middlesbrough na Birmingham City.

Kipa Aitor Engonga aliyezaliwa Figueres aliwahi kuzitumikia Malaga, Villareal na Valladolid kabla ya kutua Figueres ya Ligi Daraja la Tano Hispania.

Beki wao wa kati Igor Engonga aliyezaliwa mjini Santander na kupita Racing Santander, Celta Vigo kabla ya kutua Doxa Drama ya Ligi Daraja la Pili, Ugiriki.

Naye Luis Mesegeur aliwahi kucheza Atletico Madrid kabla ya kujiunga na Rayo Vallecano wakati huo kukiwa na beki wa kulia Esteban Obiang mwenye miaka 21 ambaye amezaliwa na kukulia kwenye kituo cha soka cha klabu ya Real Zaragoza ambaye anacheza Ibiza ya Ligi Daraja la Tatu nchini humo.

Ruben Belima anayecheza winga ya kushoto klabu ya Estoril ya Ligi Kuu ya Ureno, alizaliwa jijini Madrid miaka 27 iliyopita na kucheza Real Madrid na Domzale.

Paulo Ganet anacheza nafasi ya kiungo ambaye alizaliwa Malaga na kupitia klabu za Malaga, Rela Betis na Celta vigo huku hivi sasa akichezea Algeciras iliyopo Ligi Daraja la Tatu huko Hispania.

Kiungo nyota wa Real Union ya Ligi Daraja la Tatu Hispania, Niko Kata anayecheza nafasi ya kiungo alizaliwa jijini Barcelona na kulelewa na kituo cha klabu ya Valencia wakati huo wakiwa na winga wa kushoto, Jannick Buyla ambaye anacheza Real Zaragoza ambapo alizaliwa kwenye mji wa Zaragoza na kukulia timu ya vijana ya klabu hiyo.