Samatta kumvaa Mourinho England

Sunday February 16 2020

 

BIRMINGHAM, ENGLAND. MBWANA Samatta ameisoma hii? Chama lake jipya la Aston Villa leo Jumapili litajimwaga Villa Park kukipiga na Tottenham Hotspur na takwimu za mechi hizo zinapopigwa, Samatta akizIsoma, lazima atakuna kichwa tu.

Asikwambie mtu, Aston Villa wamekuwa wakiteswa sana na Spurs, wamekuwa wakijipigia tu. Kwenye mechi nane Spurs ilizokwenda kucheza Villa Park hawajawahi kupoteza, huku wakishinda mechi nne za mwisho mfululizo, wakifunga mabao 14. Kwenye mechi hizo, Aston Villa imefunga bao moja tu. Aston Villa hawajawahi kuichapa Spurs nyumbani tangu Januari 2008 huku ushindi wao wa mwisho ulikuwa Aprili 2015, waliposhinda 1-0 uwanjani White Hart- Lane.

Samatta ataachaje kukuna kichwa hapo? Lakini, hii ni Aston Villa mpya na Spurs sio ya Mauricio Pochettino. Spurs ya Jose Mourinho kwenye mechi 10 zilizopita walizocheza

kwenye michuano yote, mbili tu ndizo ambazo hawakuruhusu wavu wao kuguswa. Lakini, mechi nyingine nane zote wameokota mipira kwenye nyavu zao hivyo jambo hilo linampa matumaini

Samatta ya kutupia.

Spurs wanahitaji kushinda mechi hiyo ili kusogelea Top Four, lakini Aston Villa wenyewe wanatambua pia wapo kwenye hatari ya kuporomoka kwenye kundi la timu zinazochuana kutoshuka daraja, hivyo kipute hicho cha Villa Park kitakuwa cha kibabe tu. Samatta na Mourinho acha wamalizane. Spurs wataomba rekodi zao ziendelee, lakini safari hii shughuli itakuwa pevu. Rekodi zao za jumla, timu hizo mbili zimekutana mara 144, Spurs ikishinda mata 63, Aston Villa wameshinda 49 na sare ni 32 huku Spurs ikifunga mabao 242 na kufungwa 203 na Aston Villa ni kinyume chake.

Advertisement

Rekodi za msimu huu, Aston Villa wameshinda mechi saba kati ya 25 walizocheza na kuvuna pointi 25, wakitoka sare nne na vichapo 14 huku wamefunga mabao 32 na kufungwa 47. Wanashika nafasi ya 17 kwenye msimamo, pointi moja tu juu ya timu zilizo kwenye shimo la kushuka daraja. Hivyo bila ya shaka watahitaji huduma bora kutoka kwa mshambuliaji wao mpya, Samatta, ambaye ameshafunga mara moja kwenye Ligi Kuu England akiwa na wababe hao wa Villa Park.

Spurs wao wapo kwenye nafasi ya sita, pointi 37 walizovuna kwenye mechi 25, ambazo wameshinda 10, sare saba na vichapo vinane. Wamefunga mabao 40 na kufungwa 32. Pointi za Spurs ni nne tu pungufu ya kuifikia Chelsea kwenye Top Four, ambao wao shughuli yao itakuwa kesho Jumatatu, wakati watakapowakaribisha Manchester United uwanjani Stamford Bridge.

Samatta ana shughuli pevu ya kuokoa jahazi. Kikosi chake kinachonolewa na Dean Smith kimepata pointi moja tu kwenye mechi walizocheza dhidi ya timu 10 za juu kwenye msimamo, hii ilikuwa kwenye sare yao ya 2-2 dhidi ya Man United, Desemba mwaka jana. Lakini, hii leo watajaribu kuingia uwanjani kusaka ushindi wao wa pili mfululizo nyumbani kwenye mechi za ligi kwa mara ya kwanza tangu Mei 2015. Mechi zao saba walizoshinda Aston Villa wamefanya hivyo kwenye siku tofauti za wiki na kwamba, hawajawahi kushinda Jumapili, pengine hilo litatimia dhidi ya Spurs huko Villa Park leo. Lakini, shida ni kuruhusu kikosi chao kupigiwa mashuti mengi, ambapo kwa msimu huu kwenye mechi 25 walizocheza kwenye ligi wameshakumbana na mashuti 441. Kinachowapa nguvu Spurs ni kwamba kwenye mechi 22 walizocheza ugenini kwenye Ligi Kuu England hawajawahi kupoteza na timu zilizopanda daraja kwa msimu husika tangu walipochapwa 1-0 na QPR, Aprili 2012. Spurs yenyewe pia ina shida kubwa kwenye beki yao, ambapo wameruhusu mashuti 125 kupigwa langoni mwao wakati wao wamepiga mashuti 110. Mabeki wao wamekuwa na shida na kuwa timu ya kwanza kuruhusu penalti nne mfululizo tangu wafanye hivyo Stoke City Desemba 2013 hadi Januari 2014.

Mchezo mwingine wa ligi hiyo utakaopigwa leo, Arsenal ya Mikel Arteta itakuwa nyumbani Emirates kuwakabili Newcastle United. Arsenal watahitaji kushinda mchezo huo kujiondoa kwenye nafasi ya 12 wanayoshika kwa sasa, lakini Newcastle nao wakipambana kushinda ili kuzikimbia timu za mkiani kwenye mbio kazi ya kujinusuru kushuka daraja. Kipute cha kesho Jumatatu huko Stamford Bridge kitakuwa cha kibabe zaidi, Chelsea itakapomaliza ubishi na Man United, huku mechi hiyo ikiwa na taswira ya kusaka Top Four.

Advertisement