Simbu ampigia hesabu Kipchoge Olimpiki

Thursday February 13 2020

 

By Imani Makongoro, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Alphonce Simbu ameahidi kuchuana vikali na nyota wa riadha duniani Eliud Kipchoge katika mashindano ya Olimpiki yatakayoanza Julai 26, mwaka huu.

Wakati Simbu akijipanga kupamba na Mkenya huyo, mwanariadha wa kike Failuna Abdi atachuana na mshindi wa medali ya dhahabu ambaye pia anatoka Kenya Jemima Sumgong.

Simbu na Failuna watachuana na mabingwa hao watetezi wa mbio za marathoni za Olimpiki huku tofauti ya muda waliotumia kutwaa medali ukiibua hofu kama watashinda.

Kipchoge anayeshikilia rekodi ya mwanariadha mwenye kasi ya marathoni duniani ni miongoni mwa nyota watakaotoa upinzani kwa Simbu katika mbio za wanaume.

Simbu ambaye katika Olimpiki iliyopita alimaliza wa tano akitumia saa 2:11:15 aliachwa kwa dakika 2:31 na Kipchoge aliyekimbia saa 2:08:44.

“Natambua ugumu wa mashindano hivi sasa kila mmoja ameboresha muda wake, vita itakuwa kubwa lakini najipanga kurudi na medali baada ya kuikosa msimu uliopita,” alisema Simbu jana.

Advertisement

Alisema wako katika mazoezi ya wazi wakisubiri kambi ya RT ambayo wanatamani ifanyike kwa miezi minne kabla ya kwenda Japan kwenye Olimpiki.

Katika Olimpiki iliyopita, Simbu aliachwa kwa dakika 1:21 na mshindi wa medali ya fedha raia wa Ethiopia, Lilesa Feyisa aliyetumia saa 2:09:54 na dakika 1:10 na mshindi wa fedha, Rupp Galen wa Marekani aliyekimbia kwa saa 2:10:05.

Failuna atachuana na Jemima aliyekimbia kwa saa 2:24.04, mshindi wa medali ya fedha Eunice Kirwa wa Bahrain (2:24.13) na Mare Dibaba wa Ethiopia (2:24.30) aliyetwaa shaba. Failuna ana rekodi ya kukimbia kwa saa 2:27:55, akiachwa kwa dakika 3:51 na bingwa mtetezi.

Kocha wa Failuna, Thomas Tlanka alisema mwanariadha huyo ana nafasi nzuri ya kupunguza muda kabla ya kuanza mashindano hayo.

Advertisement