Vita ya makipa inavyoibeba Taifa Stars

Kipa ni nafasi nyeti kwenye mchezo wa soka na ina nafasi kubwa ya kuamua matokeo ya mchezo kwa timu kutokana na ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yake.

Timu inapokuwa na kipa mzuri na mwenye kiwango bora, mara kwa mara lango lake huwa salama na wakati mwingine inakuwa sio jambo rahisi kwa washambuliaji wa timu pinzani kufumania nyavu zake.

Kipa mbali na kulinda lango pia huwa ana majukumu mengine ambayo ni kusoma mchezo na timu yake kisha kuipanga sambamba na kuichezesha.

Hapa Tanzania katika siku za hivi karibuni kumeibuka idadi kubwa ya makipa ambao wanafanya vizuri wakileta matumaini ya kuwa msaada kwa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’.

Kundi kubwa la makipa hao ni vijana ambao ni wazi kwamba watadumu kwa muda mrefu na watakuwa tegemeo la miaka mingi kwa Taifa Stars na klabu zao wanazocheza nje na ndani ya nchi.

Klabu hizo ndizo zimekuwa chachu ya kuzalisha makipa hao ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiitumikia Taifa Stars huku wengine bado wakiendelea kuichezea timu hiyo.

Hata hivyo kufanya vizuri kwa makipa hao katika klabu zao, hakukuja kwa bahati mbaya bali ni kutokana na ushindani uliopo kutoka kwa makipa wengine katika vikosi vya timu zao ambao unawafanya wajitume zaidi, jambo ambalo linakuja kuwa na faida kwa timu ya Taifa.

Spoti Mikiki inakuletea tathmini ya namna gani ushindani au vita ya makipa kwenye ngazi ya klabu unavyotengeneza makipa bora ambao wanakuwa wameshakamilika tayari kwa kuitwa na kucheza Taifa Stars wakati wowote.

Metacha Mnata vs Farouk Shikalo-(Yanga)

Kipa Mkenya Farouk Shikalo amesajiliwa na Yanga msimu huu wakimuona kama chaguo la kwanza mbele ya wazawa wawili wenye umri mdogo ambao ni Metacha Mnata na Ramadhan Kabwili.

Hata hivyo leseni yake ya kuitumikia Yanga kwenye mechi za hatua za mwanzoni za kimataifa ilichelewa kuletwa nchini kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) jambo lililolazimu,Metacha kupewa kibarua cha kusimama langoni.

Katika mechi hizo za kimataifa ambazo Metacha amedaka, ameonyesha kiwango bora kutokana na uwezo wa kuokoa mashambulizi ya washambuliaji wa timu pinzani lakini kubwa zaidi, aliokoa mkwaju wa penalti kwenye mechi ngumu ya ugenini dhidi ya Township Rollers ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kutinga hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Uwepo wa Shikalo bila shaka unamfanya Metacha ambaye pia anadakia Taifa Stars, asibweteke na kulazimika kuonyesha kiwango bora kwani bila ya hivyo atajikuta akisotea benchi

Kana kwamba haitoshi pia ana ushindani kutoka kwa Kabwili ambaye pia amewahi kudakia Taifa Stars naye anapambana kuwa chaguo la kwanza ama la pili ndani ya Yanga.

Aishi Manula vs Beno Kakolanya- (Simba)

-Manula hakuwa na ushindani mkubwa wa namba msimu uliopita lakini ujio wa Kakolanya aliyenaswa kutoka Yanga, ni wazi kwamba utasaidia kumuimarisha na kumfanya aboreshe zaidi kiwango chake ndani ya kikosi cha Simba jambo linaloweza kumrudisha katika kikosi cha Taifa Stars.

David Kissu vs Boniface Oluoch (Gor Mahia)

Moja ya ushindani wa namba ambao utakuwa na faida kwa Taifa Stars ni ule uliopo kwenye kikosi cha Gor Mahia ya Kenya ambao unawahusisha makipa David Kissu na Boniface Oluoch.

Kukutana na kipa mahiri, Boniface Oluoch ambaye aliwahi kucheza hadi timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ kumeonekana kuwa chachu kwa kipa Mtanzania, Kissu ambaye amejiunga na Gor Mahia akitokea Singida United.

Kissu amekuwa bora kwa sasa na alitumia vyema kitendo cha Oluoch kuwa nje kutokana na majeraha, kumpoka nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Gor Mahia na ikiwa ataendelea hivyo maana yake Tanzania itakuwa na uhakika na kipa anayecheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Juma Kaseja vs Jonathan Nahimana- (KMC)

Kuna makipa wawili wazuri katika kikosi cha KMC ambao ni Juma Kaseja na Jonathan Nahimana ambaye ni raia wa Burundi.

Kiwango bora cha Nahimana ambaye ni chaguo la kwanza la timu ya taifa ya Burundi, umekuwa chachu kwa Kaseja kuweza kuimarisha na kutunza kiwango chake jambo ambalo limekuwa msaada kwa Taifa Stars katika siku za hivi karibuni.

Kaseja baada ya kuwa nje ya Taifa Stars kwa muda mrefu, safari hii amerudi tena kwa nguvu mpya akiwa ni chaguo la kwanza huku akiiweka mgongoni timu hiyo kwa kuokoa mikwaju ya penalti katika mechi mbili dhidi ya Burundi na Kenya katika mashindano ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya kuwania kushiriki Fainali za Kombe la Dunia na kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan).

Said Kipao vs Benedictor Tinoco-(Kagera Sugar)

Ndani ya kikosi cha Kagera Sugar kuna makipa wawili ambao wote wamepata fursa ya kuchezea timu ya taifa ‘Taifa Stars’ ambao ni Benedictor Tinoco na Said Kipao.

Tinoco ambaye amewahi kuichezea Mtibwa Sugar na Yanga amekuwa chachu ya kuimarisha kiwango cha Kipao ambaye kwa sasa ni chaguo la kwanza la timu hiyo.

Uwepo wa Tinoco umemfanya Kipao apambane na kuwa moto wa kuotea mbali msimu huu ambapo katika mechi tatu za mwanzo ameruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu. Pamoja na kufungwa mabao matatu dhidi ya Simba kiwango hicho kimemfanya apate uteuzi katika timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’.