Dk Msolla, Mwakalebela waula uongozi Yanga

Muktasari:

Msolla amembwaga mpinzani wake Jonas Tiboroha aliyepata kura 60, huku kura tano zikiharibika kati ya kura 1341 zilizopigwa.

Dar es Salaam. Dk Mshindo Msolla amechaguliwa kwa kishindo kuwa mwenyekiti wa klabu ya Yanga akipata kura 1276 kati ya kura 1341 zilizopigwa leo katika Bwalo la Maafisa wa Polisi, Osterbay.

Msolla amembwaga mpinzani wake Jonas Tiboroha aliyepata kura 60, huku kura tano zikiharibika kati ya kura 1341 zilizopigwa.

Msolla alisema ni deni kubwa kwa wanachama wa Yanga baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Yanga.

Msolla alisema baada ya kuangalia asilimia zilizopatikana katika kura zake ameona namna ambavyo wanachama wameonyesha kumwamini.

Hata hivyo aliongeza anajua kulikuwa na makundi mengi wakati wa uchaguzi, lakini mambo hayo yanatakiwa yawekwe pembeni.

"Yale mambo ya kambi tuyaweke pembeni kabisa na hivi sasa tunachokiangalia ni namna ya kuitengeneza klabu yetu," alisema.

Msolla alifunguka zaidi na kusema baada ya shughuli za uchaguzi kumalizika anataka wanachama wabakie na kujua namna ambavyo wataondoka kuelekea mkoani Iringa kushuhudia mchezo wa nusu fainali ya FA dhidi ya Lipuli dhidi ya Yanga.

Naye Tiboroha amempongeza mpinzani wake akisema Yanga inaelekea mahali pengine huku akidai matokeo aliyapata mapema kabla hata ya kutangazwa na kwenye uchaguzi kuna mayokeo mawili ya kushinda au kushindwa.

Tiboroha pia alitaka kambi zivunjwe na wanayanga wote sasa ni timu Msolla.

Nafasi ya Makamu mwenyekiti ni Fredrick Mwakalebela aliibuka kidedea kwa kura 1206 akiwapiku  Chota  Magege kura 12, Tito Osoro 17, Yono Kevella 31 na Janeth Mbene 64.

Mwakalebela: Ndoto Yangu imetimia

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela amesema alikuwa na ndoto ya kuongoza Yanga na sasa imetimia.

Mwakalebela ametamka hayo muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi kwenye uchaguzi wa Yanga leo.

"Tutafanya kazi kubwa kuhakikisha Yanga inafika ambapo Wanayanga wa natamani kufika,” alisema Mwakalebela.