Aggrey Morris asubiri adhabu - Bodi ya Ligi

Dar es Salaam. Baada ya nahodha wa Azam, Aggrey Morris kulalamikia upangwaji mbovu wa ratiba huku akidai timu yao kufanyiwa figisu, mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto amemwambia ameikosea bodi hiyo na asubiri adhabu yake.

Azam ililazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya JKT Tanzania juzi na baada ya mchezo huo, Morris alihojikiwa na Azam TV na kuzungumzia kuchukizwa kwake na hatua ya mchezo wao kubadilishwa kutoka saa 1:00 usiku kam ilivyokuwa imepangwa awali na kufanyika saa 10:00 jioni.

“Tulikuwa na lengo la kupata pointi tatu ili kuzikuta timu za juu lakini wakati mwingine ratiba inachangia kwani siku zote unaambiwa mechi mnacheza saa moja halafu saa tatu usiku kabla ya siku ya mchezo, mnashtukizwa na kuambiwa mechi kesho saa 10:00 jioni na wakati siku zote tulifanya mazoezi tunafanya saa moja usiku ili kuzoea hali ya hewa ya muda huo.

“Yaani kila tukishinda na tukizikaribia hizo timu za juu mbili tunaletewa figisu kama hizi. Kwa hivi tunavyoenda mpira wa Tanzania siku zote tutakuwa nyuma kwani ratiba leo unaambiwa hivi, kesho inapanguliwa unaambiwa hivi yaani ratiba unashtukizwa kama genge la samaki,” alisema Morris.

Mng’uto alisema Bodi ya Ligi ina utaratibu iliojiwekea, “huyo mchezaji hajui kama tuna sheria ngumu sana sasa hivi. Ukiwa unalalamika tu ovyoovyo ujue litakukuta la kukukuta hivyo huyo nae asubiri adhabu yake... Sisi huwa tunaongea na viongozi wa klabu hivyo mchezaji sio kiongozi wa klabu hata kama ana malalamiko anatakiwa kwenda kwenye klabu yake kulalamika klabu ituletee.”