Ajibu, Yikpe hesabu zao zimekataa

Thursday March 26 2020

 

By Charles Abel,Imani Makongoro [email protected]

Dar es Salaam. Maisha ya Ibrahim Ajibu, Yikpe Gnamien na wachezaji wengine wanne wa Yanga, Simba, KMC na Azam ni ishara tosha ya methali inayosema ‘mipango si matumizi’.

Licha ya matumaini ya kufanya vizuri waliyokuwa nayo na klabu hizo pindi walipokuwa wakisajiliwa mwanzoni mwa msimu huu, mambo yameonekana kuwa tofauti na matarajio yao.

Hadi sasa msimu ukiwa unaelekea ukingoni, wachezaji hao hawajaweza kutimiza kiu na matarajio ya wengi kama ilivyokuwa awali.

Wachezaji hao wameshindwa kuonyesha kiwango bora na kutoa mchango kwa timu, jambo lililochangia wasote benchi katika idadi kubwa ya mechi msimu huu.

Katika kundi la wachezaji sita ambao mambo yamewaendea mrama, mbali na Ajibu anayecheza Simba na Yikpe wa Yanga, wengine ni Gadiel Michael (Yanga), Richard Djodi, Abalkassim Khamis (Azam) na Salim Aiyee (KMC).

Baada ya kung’ara Yanga msimu uliopita akifunga mabao sita na kupiga pasi 14 zilizozaa mabao katika Ligi Kuu huku akiwa nahodha, Ajibu amegeuka kuwa mchezaji wa kawaida katika kikosi cha Simba ambacho amekuwa akisotea benchi katika idadi kubwa ya mechi msimu huu.

Advertisement

Mshambuliaji huyo ameanza katika kikosi cha kwanza Simba msimu huu katika mechi zisizozidi tano katika mashindano yote huku akifunga mabao mawili tu na kupiga pasi moja iliyozaa bao.

Ajibu mara kwa mara amekuwa akisotea benchi kutokana na kushindwa kufua dafu mbele ya John Bocco, Meddie Kagere, Deo Kanda, Miraji Athumani, Clatous Chama, Francis Kahata na Luis Miquissone ambao wamekuwa kipaumbele cha kocha Sven Vandenbroeck.

Ukiondoa Ajibu, majanga kama hayo yameikuta Yanga ambayo licha ya mategemeo makubwa waliyokuwa nayo wakati wanamsajili Yikpe katika dirisha dogo akitokea Gor Mahia ya Kenya, kwasasa amekuwa ni mmoja wa wachezaji wenye mwelekeo wa kuonyeshwa mlango wa kutokea klabuni hapo.

Yikpe licha ya kufunga mabao mawili Yanga, udhaifu alionao wa ubutu wa kufumania nyavu, uwezo duni wa kumiliki mpira, kusimama katika nafasi sahihi pindi wanaposhambuliwa na kushindwa kutengeneza nafasi za mabao vimemfanya asote benchi ama jukwaani katika idadi kubwa ya mechi za Yanga msimu huu akishindwa kupata nafasi mbele ya Ditram Nchimbi, Tariq Seif, Patrick Sibomana, Mapinduzi Balama na David Molinga.

Baada ya kushika nafasi ya pili katika ufungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, maisha yamekwenda kasi kwa nyota wa KMC, Salim Aiyee ambaye amekuwa na ukame wa mabao katika timu yake mpya ambayo ameifungia bao moja tu katika ligi msimu huu.

Beki wa kushoto Gadiel ambaye ilitegemewa angeleta ushindani wa hali ya juu kwa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ katika kikosi cha Simba baada ya kusajiliwa msimu huu akitokea Yanga, amekuwa akisota benchi mara kwa mara akipata nafasi ya kucheza mara chache tofauti na ilivyotegemewa.

Nako Azam wachezaji walio katika wakati mgumu licha ya matarajio ya wengi lakini wameishia kusugua benchi ni Abalkasim aliyetokea Kagera Sugar na Djodi aliyenaswa akitokea Ashanti Gold ya Ghana.

Abalkassim ambaye aliifungia Kagera Sugar mabao saba msimu uliopita, tangu ajiunge na Azam hajawahi kuifungia hata bao moja katika Ligi Kuu na amekuwa akisota benchi au jukwaani katika idadi kubwa ya mechi msimu huu.

Kauli za wadau

Mchambuzi Joseph Kanakamfumu alisema tatizo la wachezaji wa Tanzania wana mambo mengi tofauti na Ulaya.

“Wenzetu mchezaji kuendelea kuwa fiti na kucheza kwa kiwango kilekile kwa muda mrefu sababu ya mifumo ya makocha wao hapa kwetu bado tuna changamoto hiyo. “Mchezaji anapohama timu au kocha mpya anapokuja baadhi ya wachezaji mifumo inawakataa na wengine inachukua muda kuzoea,” alisema Abdallah Kibadeni.

Advertisement