Azam FC yaipunguzia kasi Simba ubingwa Ligi Kuu

Monday May 13 2019

 

By Sebastian Thobias

Dar es Salaam. Timu ya Simba imelazimishwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya Azam FC mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa leo Jumatatu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam

Suluhu hiyo ni mwendelezo wa kikosi hicho cha Patrick Aussems ambacho kimekwama kupata matokeo mazuri katika mechi zake mbili. Huo ni mchezo wa pili mfululizo baada ya ule uliopigwa mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Kagera Sugar  ambapo timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi ilifungwa bao 1-0.

Baada ya mchezo huo wa leo, Simba wapo kileleni wakiwa na alama 82, huku wakifukuzana na watani zao Yanga waliopo nafasi ya pili wakiwa na alama 80. Lakini Simba wana faida kwa kuwa na michezo mingi zaidi wanayohitajika kukamilisha kwenye ratiba yao.

Katika kipindi cha kwanza timu hizo zilizishindwa kutambiana na kuzifanya kwenda mapumziko bila kuziona nyavu za mwenzake kila upande.

Washambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere walionekana kusumbua ngome ya Azam mara kwa mara  hata hivyo safu ya ulinzi ya Azam ilionekanaa kuwa imara.

Wakati ligi hiyo ikielekea ukingoni, Kagere anaongoza kwenye wafungaji akiwa na mabao 20 huku Okwi hadi sasa akiwa na mabao 14.

Mechi zingine za Ligi Kuu zitaendelea kesho Jumanne, huku Yanga watakuwa na kibarua mbele ya Ruvu Shooting na mchezo mwingine utawakutanisha Biashara United dhidi ya Alliance FC.

Advertisement