Bondia Mtanzania aishangaza dunia

Muktasari:

  • Mwakinyo alicheza pambano la mwisho la utangulizi lililokutanisha bondia maarufu wa Uingereza Amir Khan dhidi ya Samuel Vargas.

Dar es Salaam. Bondia Hassan Mwakinyo ameweka historia mpya katika ngumi, baada ya kumchapa mpinzani wake Sam Eggington wa Uingereza.

Mwakinyo alicheza pambano la mwisho la utangulizi lililokutanisha bondia maarufu wa Uingereza Amir Khan dhidi ya Samuel Vargas.

Khan alishinda kwa pointi pambano hilo baada ya kupata upinzani mkali kutoka kwa Vargas.

Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana, Mwakinyo alisema haikuwa kazi rahisi kupata ushindi huo kwa kuwa mpinzani wake alikuwa bondia mwenye rekodi bora.

Alisema siri kubwa ya kupata ushindi ilitokana na ujasiri ndani ya ulingo akiamini kuwa anaweza kushinda licha ya kucheza na mzungu.

Bondia huyo alisema kuwa muda mfupi baada ya kumsoma Eggington, aliweka dhamira ya kumshinda kwa ‘KO’ au ‘TKO’.

“Sikutaka kumchelewesha nilijua kama tutamaliza raundi zote 10, basi majaji wangemlinda na kumpa mwenyeji ushindi, sikutaka iwe hivyo kwa hiyo niliingia ulingoni nikiwa na malengo,” alisema Mwakinyo.

Bondia huyo alisema baada ya kupata taarifa anakwenda kuzichapa katika pambano la utangulizi dhidi ya Khan, alianza maandalizi kwa takribani miezi miwili kabla ya kwenda Uingereza.

“Nilitaka heshima na kuitangaza nchi yangu, nilipopata ofa ya pambano nilijiandaa kwa miezi miwili nikiwa kambini Tanga,”alisema Mwakinyo.

Awali, alisema alihofu ubora wa mpinzani wake kabla ya kuandaliwa vyema kisaikoloji na kocha wake Rashid Nassor aliyeongozana naye katika pambano hilo.

Mwakinyo alisema kocha wake alimwambia ana kazi ngumu ya kupeperusha vyema bendera ya Tanzania na hapaswi kuogopa atakapokuwa ulingoni.

Kabla ya pambano hilo, Muingereza huyo alikuwa na rekodi ya kushika nafasi ya nane kwa ubora duniani kati ya mabondia 1800 wa uzito wa ‘super welter’ na Mwakinyo nafasi ya 175.

“Unajua huku Uingereza hakuna aliyetarajia bondia kutoka Tanzania kama Mwakinyo angeshinda, waliamini angepigwa KO mbaya na hata ukumbini kabla ya pambano walimzomea wakiamini atapigwa mapema,” alisema kocha huyo.

Pambano lenyewe

Mwakinyo alithibitisha ubora wake katika raundi ya pili alipowaduwaza Waingereza kwa ngumi kali zilizomchana sehemu ya mdomo mpinzani wake katika pambano hilo lililopigwa kwenye Ukumbi wa Barclaycard Arena katika mji wa Birmingham.

Mwakinyo akionekana imara ulingoni, alimshushia makonde mpinzani wake mfululizo kabla ya kuokolewa na mwamuzi Kevin Parker.

Mwamuzi huyo alilazimika kumuokoa Eggington baada ya kupigwa ngumi 51 bila majibu katika raundi ya pili huku maelfu ya mashabiki waliofurika ukumbini hapo wakiwa kimya wasiamini kilichotokea.

Mkanda wa video wa pambano hilo ulionyesha ushindi wa Mtanzania ulianza kuonekana raundi ya kwanza, baada ya kumtandika mpinzani wake konde kali la kulia lililompata vyema mdomoni na kumpasua.

Eggington alilazimika kutumia dakika moja ya mapumziko katika kona yake kutibiwa ili kupunguza maumivu ya konde la raundi ya kwanza kitendo ambacho kiliamsha morali ya Mwakinyo ambaye alitumia muda huo kuzunguka kwenye kona zote za ulingo akitamba.

Raundi ya pili, Mwakinyo alianzisha mashambulizi huku mpinzani wake akijihami na kurusha ngumi za kushitukiza kabla ya kugeuziwa kibao na mwamuzi alilazimika kumukoa na kutangaza matokeo ya ushindi wa ‘Technical Knock Out’ (TKO) kwa Mtanzania.

Bondia wa zamani wa timu ya Taifa, Emmanuel Mlundwa alisema dunia imepata mshituko kutokana na ushindi huo.

“Kitendo cha kumpiga bondia namba nane kwa ubora duniani, sio kitu kidogo, hata Waingereza hawakutarajia hilo, ushindi wake ni rekodi nzuri kwa mabondia wetu.

“Nimeliangalia pambano la Mwakinyo, kwanza hakuwa na hofu tangu anapanda ulingoni licha ya umati mkubwa wa mashabiki alionekana kujiamini na amejiandaa,”alisema Mlundwa.

Alisema ushindi huo ni funzo kwa mabondia wasiokuwa na majina nchini kujifunza kupitia Mwakinyo kwa kujiandaa vyema wanapocheza nje ya nchi.

Bondia huyo ameandaliwa pambano la ubingwa wa kimataifa wa IBF kwa vijana uzani wa ‘super middle’ dhidi ya Wanik Awdijan Oktoba 20 Ukumbi wa Alex Sportcentrum ulioko Nuremberg, Ujerumani.