Dakika hizi hatari kwa Simba

Friday March 8 2019

 

By Eliya Solomon, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Nafasi ya Simba kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ipo mikononi mwa kipa Aishi Manula na mabeki wake endapo watakuwa makini zaidi katika dakika 45 za mwisho dhidi ya JS Saoura.

Simba itashuka uwanjani Jumamosi saa 4:00 usiku kuhakikisha inapata sare au ushindi ili kusonga mbele katika mashindano hayo.

JS Saoura inayoshika nafasi ya tatu katika Kundi D kwa pointi tano, imeonekana kuwa tishio kipindi cha pili ambacho imekuwa ikifunga idadi kubwa ya mabao kulinganisha na dakika 45 za kwanza.

Rekodi za mechi 10 zilizopita zinatoa picha ya wazi namna Saoura ilivyo hatari katika dakika 45 za mwisho za mchezo.

JS Saoura imefunga mabao manane katika mechi 10, jambo litakalomlazimu Kocha Patrick Aussems kutumia mfumo bora wa kujilinda hasa kipindi cha pili.

Pamoja na Simba kuwakosa mabeki Juuko Murshid na Erasto Nyoni bado tumaini lake litakuwa kwa Paul Bukaba kushirikiana vyema na Pascal Wawa.

Advertisement

Rekodi zinaonyesha katika mabao manane waliyofunga JS Saoura katika mechi 10 za hivi karibuni ni bao moja pekee walifunga kipindi cha kwanza tena ilikuwa Januari 22 kwenye mchezo wa Ligi dhidi ya Oran na bao hilo lilifungwa na mshambuliaji wake nguli Yahia Cherif.

Mabao saba waliyopata kipindi cha pili, manne ni kati ya dakika 75 hadi 90 dhidi ya Tadjenant ya Ligi Kuu walioshinda 2-0 na moja kati ya hayo likifungwa na Ulimwengu dakika ya 82.

Mengine waliichapa AS Vita ya DR Congo katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika mchezo wa kwanza walitoka sare 2-2. Bao lao la kusawazisha lilifungwa dakika ya 88 na Cherif mwenye miaka 34.

Pia, katika mchezo wa marudiano uliochezwa Februari 12 nchini Algeria dhidi ya AS Vital bao la Ziri Hammar lilitosha kuwafanya kuibuka na ushindi huo mwembamba.

Mabao mengine matatu walifunga kipindi cha pili mawili kati ya hayo ni dakika kati ya 45 hadi 60, la kwanza lilikuwa dhidi ya AS Vita, lilikuwa bao lao la kwanza kwa upande wao lililofungwa dakika ya 45 kwa penalti katika sare ya 2-2.

Bao jingine ilipata katika mchezo wa Januari 18 lililofungwa na mkongwe Cherif katika matokeo ya sare ya bao 1-1 na Al Ahly.

Bao la mwisho kati ya hayo matatu yalifungwa dakika 60 hadi 75 Februari 7 ambapo wapinzani wao Hussein Dey wajifunga dakika ya 70.

Habari njema kwa Simba ni kuhakikisha washambuliaji wake wanatumia vizuri udhaifu wa safu ya ulinzi ya Saoura ambayo imeruhusu mabao karibu katika kila mchezo.

Rekodi zinaonyesha timu hiyo inayoundwa na mshambuliaji wa Tanzania, Thomas UIimwengu imefungwa mabao 11, kipindi cha kwanza.

JS Saoura katika mechi 10 zilizopita kati ya mabao 11 waliyofungwa, sita walifungwa kipindi cha kwanza kati ya dakika 30 hadi 45.

Mabao mengine wamefungwa kipindi cha pili dakika 45 hadi 60 (2), 60 hadi 75 (1) na 75 hadi 90 (1).

Simba katika mechi 10 imefunga mabao 17 na kufungwa tisa katika mashindano yote yakiwemo katika mchezo miwili ya Kombe la Sportpesa dhidi ya Bandari ya Kenya na Mbao FC.

Kauli ya Chambua

Kocha Sekilojo Chambua alisema Simba inatakiwa kucheza kwa nidhamu hasa katika eneo lake la ulinzi kwa kuwa timu hizo zinajuana.

“Simba ikacheze kwa tahadhari muda wote wa mchezo licha ya kwamba waliwafunga mabao 3-0 haina maana ni wabovu. Mabeki wawe macho kwa kucheza kwa umakini,”alisema nyota huyo wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa, Taifa Stars.

Advertisement