Diamond aahidi kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro

Msanii wa Bongofleva nchini Tanzania, Diamond Platnumz

Muktasari:

Msanii wa Bongofleva, Diamond Platnumz  amewasili Wilayani Moshi na kuahidi kupanda mlima Kilimanjaro hadi kileleni.

Moshi. Msanii wa Bongofleva nchini Tanzania, Diamond Platnumz ametua Marangu wilayani Moshi Mkoa wa Kilimanjaro na kuahidi kupanda mlima Kilimanjaro hadi kileleni, safari inayoanza leo Jumamosi Septemba 28, 2019.

Akizungumza jana Ijumaa Septemba 26, 2019 muda mfupi baada ya kuwasili wilayani humo, Diamond alisema safari hiyo itakayochukua takribani siku tano, alitamani kwenda siku moja na kurudi.

Hata hivyo, alisema kutokana na ushauri wa Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Dk Hamis Kigwangalla ambaye ndio mwenyeji katika kampeni ya 'Kili Challenge Twenzetu Kileleni" alimtaka aambatane na watu wengine zaidi ya 130 watakaopanda mpaka wote wafike sawa.

 "Mimi uwezo wa kupanda mlima siku moja ninao kwani ni sawa na shoo yangu moja, narudi nawaacha kina Mwana FA wakijikongoja," alisema Diamond  

Hata hivyo, hakusita kumwagia sifa Waziri Kigwangalla kwa ubunifu wake wa kuwatumia wasanii na kuongeza ni wakati wao sasa kutangaza vivutio vinavyopatikana hapa nchini kwa kuwa wameshakuwa mabalozi wa bidhaa mbalimbali hivyo hilo ni jambo dogo kwao.

Kwa upande, wake msanii MwanaFA, alisema pamoja na nchi kujaliwa vitu vizuri ambavyo havilipiwi kwa Mungu ukweli ni kwamba wasanii bado hawajafanya kazi yao ipasavyo. 

MwanaFA alisema ni wakati sasa suala la kutangaza vivutio vya utalii kulichukulia kama sheria kwao  na kulizungumzia kila wanapokwenda.

Msanii Jacob Steven, maarufu kwa jina la JB, amesema watu wamekuwa wakimtisha na mwili wake kuwa hatafika kileleni lakini atawaonyesha maajabu na kuwa msaada kwa wengine. 

"Kuna watu wamekuwa wakisema wanene kama sisi hatuwezi kupanda mlima huo, lakini wazoefu wa huku wamenihakikishia kwamba kupanda mlima sio kuwa na mwili mwembamba, hivyo nina imani hata mimi nitafika kileleni," alisema JB