Eymael, msaidizi wake wajifunga Yanga miezi 18

Muktasari:

Eymael ni mmoja kati ya makocha wakubwa Ulaya mwenye uzoefu wa kufundisha soka la Afrika, akiwahi kutwaa mataji kadhaa akiwa na timu tofauti Afrika katika nchi za DR Congo, Gabon, Afrika Kusini, Rwanda na Kenya.

Dar es Salaam.Kocha Mkuu mpya wa Yanga, Luc Eymael na msaidizi wake Reidoh Berdien wamesaini mikataba ya mwaka mmoja na nusu kila mmoja.

Makocha hao wamesaini mikataba hiyo leo mbele ya Mwenyekiti wa klabu hiyo Dk Mshindo Msolla aliyeambatana na mwanasheria wa klabu hiyo Simon Patrick.

Eymael sasa rasmi anachukua nafasi ya Mkongomani Mwinyi Zahera ambaye alitupiwa virago mwisho wa mwaka jana.

Jukumu kubwa la Eymael sasa litakuwa ni kuhakikisha Yanga unachukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho na kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya Afrika msimu ujao.

Baada ya kumalizana na Eymael pamoja na Berdien ambaye ni kocha namba mbili akiwa ni mtaalam wa mazoezi ya viungo klabu hiyo sasa ipo katika mazungumzo na kocha atakayekuwa kocha msaidizi wa kwanza.

Taarifa za uhakika ni kwamba Yanga ipo katika hatua za mwisho kumalizana na kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime ambaye anahitajika klabuni hapo kuwa msaidizi wa kwanza wa Eymael.