Huyu ndiye mchezaji aliyesajiliwa Simba kwa nauli ya daladala

Moses Mkandawile anaingia katika kitabu cha makipa bora waliowahi kutokea baada ya kutamba na kikosi cha Simba katika miaka ya themanini.

Bila kutaja jina la Mkandawile katika orodha yako ya makipa bora hutakuwa umelitendea haki soka la Tanzania katika eneo la kipa.

Mkandawile ni miongoni mwa wachezaji waliovuma miaka ya themanini akiwa mmoja wa makipa mahiri aliyekuwa tishio uwanjani.

Nguli huyo aliyekuwa na urefu unaokadiriwa kuwa mita sita, anaingia katika orodha ya makipa hodari akiungana na Omari Mahadhi, Athumani Mambosasa, Joseph Fungo, Sahau Kambi, Kichochi Lemba, Madata Lubigisa na wengine waliofanya vyema kwa nyakati tofauti.

Pamoja na ubora wa makipa hao niliotaja, lakini Mkandawile ana sifa ya ziada, ndiye kipa aliyeinusuru Simba kuteremka daraja mwaka 1987.

Ilikuwa hivi. Simba haikuwa na namna zaidi ya kushinda mechi dhidi ya watani wao wa jadi Yanga kupata sare au kipigo kilikuwa kinaishusha daraja timu hiyo.

Mkandawile ndiye aliyesimama langoni katika mchezo huo na kuisaidia Simba kupata ushindi wa mabao 2-1 yaliyofungwa na Edward Chumila na John Makelele ‘Zigg Zagg’. Nahodha Issa Athumani ‘Sekatawa’ alifunga kwa upande wa Yanga.

Kumbukumbu haiwezi kufutika katika historia ya klabu hiyo kwani haikuwa kutokea Simba kucheza chini ya kiwango kiasi cha kuhatarisha nafasi yake ya ushiriki wa mashindano hayo.

Mkandawile aliyekuwa kipa namba moja wa Simba baada ya mtangulizi wake Idd Pazi kufungiwa na FAT (sasa TFF), usajili wake ndani ya klabu hiyo ni simulizi inayofurahisha.

Akizungumza na Spoti Mikiki, Mkandawile alisajiliwa na Simba kwa kupewa nauli ya daladala tu tofauti na umaarufu wake katika medani ya soka.

Yanga, Simba

Wakati kukiwa na taarifa zisizo rasmi kuwa Yanga iliikoa Simba isishuke daraja kwa kukubali kufungwa na watani wao wa jadi, Mkandawile anaweka bayana kilichotokea katika mchezo huo ambao hadi leo umebaki katika historia ya miamba hiyo.

“Ni kweli mchezo wa mwisho kati ya Simba na Yanga ulikuwa unaamua hatima yetu, tushuke daraja au kubaki, kama tungefungwa basi safari ya Simba ndiyo ingeishia hapo. Kimsingi tulitakiwa kushinda kwa namna yoyote ile hasa ukizingatia tulitoka Mwanza tukiwa tumefungwa bao 1-0 na Pamba.

“Tulifika Dar Jumanne kwa treni na mechi ilikuwa Jumamosi tukaunganisha kambini Kimara, wakati ule ilikuwa nje ya mji porini ingawa kulikuwa na hoteli moja nzuri ambako tulikuwa tukiweka kambi na mazoezi tulifanya Chuo Kikuu Mlimani (UDSM),” anasema.

Mkandawile anasema ingawa Simba ilikuwa katika mazingira magumu, Yanga ilitakiwa kushinda mechi hiyo ili kutwaa ubingwa, hivyo ilikuwa ni mechi muhimu kwa timu zote.

“Siku ya mechi tulikwenda uwanjani tukiwa na morali na mpira ulivyoanza dakika ya 10 Yanga ilipata bao lililofungwa na Issa Athumani aliyepata pasi ya mpira wa adhabu uliopigwa na Fred Minziro. Dakika chache Edward Chumila alisawazisha kabla ya John Makelele kufunga la ushindi.

“Nakumbuka bao lile mpira ulimtoka kipa wa Yanga, Sahau Kambi baada ya kurushwa wa Twaha Hamidu ukamgonga Chumila kichwani kwa nyuma akiwa jirani na goli na alipoudaka ukamponyoka na kumkuta Makelele akafunga,”anakumbuka.

Anasema matokeo hayo yaliinusuru Simba kushuka daraja, lakini yalikuwa mwiba mchungu kwa Yanga baada ya kukosa ubingwa ambao ulichukuwa na Coastal Union ya Tanga.

David Ngonya

“Chanzo cha timu kutaka kushuka ilikuwa hivi, baadhi ya watu walitaka Katibu Mkuu David Ngonya ajiuzulu lakini aligoma alisema hawezi kutoka na kuicha timu katika hali ile.

“Ngonya alikuwa na misimamo kweli hakutoka ingawa mgogoro ulikuwa mkubwa siku ya mechi wote tuliambiwa tucheze kwa nguvu zote ndiyo hatima yetu, pia wachezaji tuliambizana hakuna kuweka historia ya kuwa wachezaji ambao tumeishusha Simba daraja,”anasema.

Usajili Simba

Kumbe alianzia hapa

Mkandawire anasema katika maisha ya soka hawezi kumsahau aliyekuwa mchezaji wa kiungo wa timu hiyo Nico Njohole kwani ndiye aliyemtoa katika timu za mtaani.

“Ilikuwa siku ya Jumamosi nikiwa kazini (Uhamiaji) Njohole alikuja ofisini akaniambia Mkandawile Simba tuna mechi ya kirafiki ya kimataifa na timu ya Sweden lakini makipa wetu (Mahadhi Omari na Athumani Mambosasa) wote hawapo twende ukatusaidie kudaka.

“Tulikuta wachezaji wanaulizana nani atadaka? Njohole akawambia nimekuja na kipa mzuri tu, hivyo wasiwe na wasiwasi safari yangu kujiunga Simba ndivyo ilianza,” anasimulia.

“Kipindi tulicheza kwa mapenzi kwahiyo sikupata kitu zaidi ya kulipwa pesa ya nauli ya daladala kwenda mazoezini na kurudi nyumbani.

“Niliendelea kwenda kufanya nao mazoezini siku moja Simba ikaleta kocha raia wa Brazil aliponiona mazoezini alivutiwa na kiwango changu akapendekeza nisajiliwe.

Anasema baada ya usajili timu ilikwenda kambini Brazil kwa siku 45 na yeye akiwa kipa namba tatu nyuma nyuma ya Idd Pazi na James Kisaka.

“Tukiwa Brazil ikaletwa taarifa Pazi amefungiwa na TFF mwaka mmoja kwa kusajili timu mbili tofauti ya Majimaji na Simba hivyo kuanzia pale mimi ndiyo nikawa namba moja. Mechi ya kwanza kudaka ilikuwa na Reli Morogoro, CDA Dodoma na Yanga baada ya hapo nikawa kipa namba moja,”anasema Mkandawile.

Ushirikina

Mkandawile anasema ushirikina katika soka upo na alitoa mfano katika moja ya mechi ambayo Simba ilicheza dhidi ya Yanga alipewa jukumu la kusimamia mchakato huo.

“Kuna siku nakumbuka nilifuatwa usiku nikaambiwa mimi kipa natakiwa nikasomewe dua, sijakaa sawa nikafuatwa tena niende nikavunje nazi.

“Niliwagomea muda huo ilikuwa saa sita usiku nikawambia siwezi kufanya hivyo napaswa kupumzika kujiandaa na mechi ya kesho hayo mambo wakafanye wenyewe sikuamka.

“Kuna mechi moja tulicheza na Coastal Union nilikuwa nahodha kuna wachezaji wakanifuata wananiuliza mbona kimya leo hatuendi ‘kutengenezwa’? tunacheza na Coastal wale wanatokea Tanga hivyo lazima tujilinde.

“Nikawajibu subirini muda bado nilichokifanya nikatoka nikaenda ofisi kwa katibu tukachukua vikaratasi tukachana nikarudi navyo kambini kufika nikamgawia kila mmoja nikawaambia wavae ndani ya njumu, ile mechi tulishinda,” anasema.

Moja ya mechi ambayo Mkandawile anaikumbuka ni Klabu Bingwa Afrika (Ligi ya Mabingwa Afrika) dhidi ya Al Ahly ya Misri.

“Tulianzia nyumbani CCM Kirumba tukashinda mabao 2-1 tukaenda kurudiana Misri, aliyekuwa Balozi wetu Sued alitukataza kwenda hotelini tukafikia nyumbani kwake mechi ilipokwisha ndipo tukaenda hotelini kusubiri siku ya safari kurudi nchini.

“Walihisi nimefanya ushirikina dakika ya 15 baada ya mechi tulishambuliwa sana lakini nilisimama imara shabiki mmoja akashuka jukwaani akaja mpaka golini kunikagua.

“Yule shabiki alikagua goli akatikisa nyavu wakati mechi inaendelea hadi aliporidhika akaondoka hakuna askari aliyembugudhi.

“Walihisi nimefanya ushirikina sababu wakati tunaingia uwanjani nilivua glovu na kuzitupia golini kwetu, kisha nikaenda kuzichukua na kuzivaa, hivyo tukio lile walihisi nimeroga lakini ilikuwa kuwaadaa tu,” anasema.

Maisha binafsi

Mkandawile aliyeanza soka akiwa shule ya Msingi Kibasila mwaka 1968 kabla ya kujiunga na Uhamiaji hivi sasa anafanya biashara ya Pub aliyoipa jina la Double M huko Barakuda, Dar es Salaam.

Anasema baada ya kustaafu soka mwaka 1990 wakati huo akiwa katika kiwango bora alilazimika kurudi darasani kwani kazi aliyokuwa akiifanya ilimlazimisha kufanya hivyo.

“Simba walinifuata na kunitaka niendelee na mpira, lakini niliwakatalia shule na mpira nisingeweza, lazima ningeshindwa baada ya masomo nilikuwa Ofisa Utumishi na Utawala Chuo cha Bima Mikocheni hadi nilipostaafu mwaka 2009.