JAMVI LA KISPOTI : Zahera ameshachelewa kuwalipua viongozi

Thursday November 7 2019

 

KUNA filamu moja inaendelea pale Yanga. Wenye mamlaka wameshatangulia wavuni kwa bao la mapema wakilifuta benchi zima la ufundi akiwemo Kocha Mwinyi Zahera ambaye ni msimu uliopita alikuwa shujaa wa timu hiyo.

Uamuzi wa Yanga kumtosa Zahera lilikuwa ni suala la wakati tu kama ambavyo nilikuwa nikisema na sasa tayari mambo yako hadharani.

Hata kama Yanga imeondoa makocha wote hilo halijawa suluhishi inachotakiwa ni kutuliza akili katika kutafuta wale watakaochukua nafasi ya wanaotoka hasa wakati huu ambao timu ipo katika mashindano.

Yanga inatakiwa kutuliza akili hasa katika kutafuta makocha wapya kwani kama mchakato huo utakuwa umelenga kama ambavyo inavyoundwa sekretarieti ya timu, basi anguko la timu litakuwa kubwa kuliko haya ya sasa ambayo Zahera anayaacha katika ukomo wa utawala wake.

Maamuzi ya mwisho ndani ya Yanga yanaonekana ni changamoto kubwa ambao inaweza kuuangusha uongozi wa klabu hiyo. Muhimu ni kujitathimini zaidi kuanzia hapa kabla ya kuangalia mbele.

Tuachane na hayo ebu tuangalie sasa maisha ya baada ya Zahera kutimuliwa kama kawaida yake, ameshindwa kuziba mdomo amemwaga mambo hadharani kwa kuwashambulia viongozi wake.

Advertisement

Zahera sasa amekuwa anafanya ziara ya kupasua yale ya ndani ya klabu hiyo hakuna anachotaka kuacha. Ameamua kusambaza ukweli lakini swali la kujiuliza uamizi wake huo una afya gani kwasasa?

Kama kutakuwa na wanachama wanaojua thamani yao watahitaji ufafanuzi juu ya haya mambo yanayoelezwa na Zahera kwa kuwa yanachangamoto zake katika maslahi ya klabu yao.

Lakini kwa upande wa pili, naona kama kocha huyo amechelewa kumwaga mboga katika kipindi hiki ambacho tayari ameshapoteza kazi. Watu wenye fikra nyepesi wataona kama ameamua kujisafisha baada ya kupoteza kazi kufuatia uamuzi wa uongozi wake kumshtua.

Upande mwingine najaribu kumshangaa na kumkumbuka Zahera wa nyuma ambaye wakati fulani alilipuka kwa uongozi uliopita kushindwa kumsajilia vyema na kuita vyombo vya habari na kuwashambulia vikali.

Zahera yule sasa hayupo amesubiri ametimuliwa ndiyo ameanza kuzungumza hatua ambayo haina tofauti na makocha tuliowazoea. Swali kwanini alisubiri zaidi hadi apoteze kazi?

Zahera alitakiwa kuyasema haya akiwa ndani pengine angeisaidia zaidi Yanga kwani wakati wote mpaka inafikia hatau ya kupigwa na makopo hakuthubutu kuyasema itachukua muda watu kukubali hili.

Kama kweli alikuwa na nia ya kuisaidia Yanga alitakiwa kuyamwaga yote haya akiwa ndani kwani yangeisadia Yanga kuwajua viongozi wabovu ndani ya klabu hiyo ambao wanaweza kuwa chanzo cha anguko la uongozi wa Dk Mshindo Msolla.

Nililisema hili katika makala zangu mbili zilizopita hakuna kinachoweza kufichika kwamba wako baadhi viongozi wabovu katika uongozi wa sasa katika klabu hiyo kongwe. Wameonyesha kuchemsha mapema na nina mashaka hawataweza kumsaidia Msolla au watampoteza zaidi.

Ukiyafuatulia mambo yanayosemwa na Zahera yanakupa wasiwasi jinsi mambo magumu yalivyo ndani ya Yanga lakini, je, yana uhalisia huo kiasi cha Yanga kulazimika kutumia mabasi ya timu pinzani?

Kama kulikuwa kunatoka pesa za majukumu hayo hawa ambao walikuwa wanatangulia mbele fedha hizo zilikuwa zinafanya majukumu gani badala ya kuhakikisha wachezaji wamekula vyema na kusafiri salama ?

Haya ni maswali ambayo Wanayanga na klabu yao wanapaswa kujiuliza na kupata majibu ya uhakika kwani yanaleta picha ambayo sio nzuri.

Na kama Zahera anasema uongo nyaraka za malipo zinaweza kusaidia kuthibitisha haya na kumhukumu Zahera kwamba anatafuta njia ya kujitetea.

Uongozi wa Yanga unatakiwa kuanza kuishi kwa umakini kutokana na kauli hizo za Zahera. Kwani mambo haya anayofunguka yanaweza kuwa mwarobaini mzuri ambao kama kuna shida ndani unaweza kutumika kutibu maradhi kwa manufaa ya Yanga.

Ukiyatafari haya za Zahera kwa kina unaweza kubaini kuwa wapo watu wameingia Yanga kwa manufaa yao binafsi. Tena unaweza kubaini kuwa Yanga imetolewa katika mashindano ya Afrika kwa mkono wa watu ambao wako ndani ya uongozi wa klabu hiyo.

Haya si mambo madogo ya kuyaacha yapite hivihivi ingawaje msemaji wake, Zahera yuko nje ya timu. Ingawaje Zahare amechelewa sana kuyaweka wazi.

Advertisement