Jeuri ya Mo Dewji atuma salamu kwa watekaji

Muktasari:

  • Muda mfupi baada MO kuposti picha hiyo, mtandao unaoaminika kule Nigeria wa Pulse, uliandika kuwa MO amenunua gari hilo kwa dola za Marekani 35,000 (Sh80 Milioni). Hata hivyo, mtandao wa Tesla wenyewe unaandika kuwa Model 3 inauzwa dola 46,000 (Sh106 Milioni).

BILIONEA mshkaji zaidi Bongo, Mohammed Dewji bila shaka sasa hivi amepata dawa ya wale wahuni wanaochafua hali ya hewa kwa kuteka watu.

Kwani hujui? Oktoba 11, mwaka huu, MO akiwa gym ya Hoteli ya Colosseum, Oysterbay, Dar es Salaam, alipokwenda kujiweka sawa kwa mazoezi, alitekwa na wahuni na kushikiliwa kwa siku nane kabla ya kumwachia.

Jinsi tukio la MO kutekwa lilivyotendeka, ripoti za kipolisi na namna alivyoachiwa, ni ishu ambayo imewaacha Wabongo wanaona nyotanyota tu. Hawakuelewa, hawajaelewa na haionekani kama utafika wakati wataelewa na kukubali kilichotokea.

Imeshagota miezi miwili tangu MO alipotokewa na kisanga cha kutekwa. Jumapili iliyopita, MO kupitia akaunti zake za Facebook, Twitter na Instagram, aliposti picha akiwa kwenye gari, akaandika maneno “Time for Something New”, kwa Kiswazi alimaanisha muda wa kitu kipya, akaambatanisha hashtag ya #HappySunday. Naam, ilikuwa Jumapili ya furaha.

Kweli ni muda wa kitu kipya. Tena kitu baabkubwa! Gari aliloposti akiwa ndani yake ni Tesla Model 3 (Tesla M3). Gari la Kimarekani. Gari linalosifika kuwa la kiusalama zaidi kuliko mengine yote duniani.

Muda mfupi baada ya MO kuposti picha hiyo, mtandao unaoaminika kule Nigeria wa Pulse, uliandika MO amenunua gari hilo kwa Dola 35,000 za Marekani (Sh80 milioni). Hata hivyo, mtandao wa Tesla wenyewe unaandika Model 3 inauzwa Dola 46,000 (Sh106 milioni).

KUHUSU TESLA M3

Tesla Model 3 ni gari linalozalishwa na Kampuni ya Tesla Inc ambayo yenyewe imejikita kutengeneza magari yasiyotumia mafuta. Magari ya Tesla yanatumia gesi na umeme tu.

Tesla Inc walianza uzalishaji wa magari hayo ya kutumia gesi na umeme tangu mwaka 2012. Gari la kwanza kutengenezwa na kampuni hiyo ni Tesla Model S, lililozalishwa mara ya kwanza mwaka 2012 na linaendelea kuzalishwa mpaka leo huku likiboreshwa kiteknolojia. Gari la pili ni Tesla Model X, lililoingizwa sokoni tangu mwaka 2015.

Kwa mujibu wa taasisi ya utafiti ya Navigant, mpaka sasa Tesla wameshauza magari karibu 500,000, yakiwa ni asilimia 20 ya magari yote yenye kutumia gesi na umeme duniani. Model S ndilo limeuzwa zaidi likiwa linamilikiwa na watu 250,000 duniani. Model X lina watumiaji 106,689 na Model 3 mpaka Oktoba mwaka huu, lilikuwa na watumiaji 100,000.

Mtandao wa US News katika ripoti yake waliyoiita “10 Safest Car Brands”, yaani Brandi 10 za magari salama zaidi, wanayataja magari ya Tesla Model 3 na Model X nafasi ya tatu. Wanayaweka magari ya Genesis G80 na G90 nafasi ya kwanza na Volvo S90 na V90, matoleo ya mwaka huu yakiwa namba mbili.

Hata hivyo, Tesla wenyewe wanatamba kwa muundo wake na mifumo ya kiusalama iliyowekwa, hakuna gari lenye kumhakikishia usalama mmiliki, dereva na hata abiria kama magari ya Tesla, hasa Tesla Model 3.

USPESHO WA TESLA M3

Halina injini kabisa. Gari lote ni umeme. Halina muungurumo. Linatembea kimyakimya, kama huelekezi macho lilipo, litapita nyuma yako pasipo wewe kujua kama kuna gari limekupita.

Lina camera za dashboard, yaani dashcam. Zenyewe huchukua matukio yote mbele, nyuma na pembeni kuzunguka gari. Ni kamera za mzunguko wa nyuzi 360 na huchukua video zenye ubora wa hali ya juu, yaani HD.

Kwa mantiki hiyo, kama MO angekuwa anatumia Tesla Model 3 kipindi kile alipovamiwa na watekaji Hoteli ya Colosseum, maana yake sasa hivi gari hilo lingerekodi matukio yote, na pengine watekaji wangejulikana kwa picha zao siku ya kwanza.

Huu ni ujumbe murua kabisa kwa wale watekaji, dawa yao ndio imepatika hivyo.

Sifa nyingine ni Tesla Model 3 ni gari kamili la kidigitali. Halina ufunguo, linatumia rimoti yenye umbo la gari lenyewe. Ukishaingia kwenye gari, kwenye dashboard kuna kitu mfano wa tablet. Hiyo ndiyo unaitumia kuendesha gari.

Ukiamua hata hiyo rimoti yake si muhimu sana. Unaweza kuweka App ya gari kwenye simu, kisha utaitumia simu yako kuendesha gari, kufungua milango, kufunga na kulidhibiti.

Tesla Model 3 lina mfumo wa autopilot ya kiwango cha juu kama ndege. Autopilot huwezesha ndege kujiongoza yenyewe ikiwa angani kwa kutambua sehemu hatari kupita na kuchagua uelekeo salama.

Kwa Tesla Model 3 kuwa na autopilot, inalifanya gari hilo kujiendesha lenyewe. Lina kamera za kutosha zenye kuona mbali (autopilot cameras), hivyo hata dereva akilikimbiza, lenyewe hutambua hali halisi ya barabara mbele ya safari, kwa hiyo hupigia kengele ya alarm. Dereva asipotii, gari lenyewe hufunga breki. Gari lina automatic break.

Gari haliwezi kugonga. Unaweza kuliendesha hata ukiwa umelala, maana likikaribia kugonga gari lingine au kitu chochote, linaona na kufunga breki lenyewe (umeambiwa lina automatic break). Ni gari ambalo limepiga hatua kubwa kufikia kiwango cha kuwa gari lenye kujiendesha bila dereva.

Kuna twiti ya CEO wa Tesla, Inc, Elon Musk mwaka juzi, wakati Tesla Model 3 likiwa katika matengenezo, alisema gari hilo likifika sehemu, kabla ya dereva kuamua kupaki, lenyewe ndilo litamwelekeza dereva sehemu ya kupaki.

Musk alisema, Tesla Model 3 haliwezi kuibiwa kabisa. Kwani katika dashboard limefungwa kitu kinaitwa Smart Summon. Kwa hiyo popote pale litakapokuwa, mmiliki wa gari kwa kutumia rimoti au simu yake yenye App ya Tesla Model 3, ataweza kuliita gari, hata likiwa nchi nyingine. Kumbuka linaweza kutembea bila dereva.

Magari ya Tesla huchajiwa kwenye vituo vya kuongeza nishati vinavyoitwa Supercharger Stations. Marekani na Ulaya vipo. Afrika hakuna kituo cha supercharger. Hata hivyo, MO akilileta nchini, hatakuwa na namna zaidi ya kuleta wataalamu ili wamfungie mfumo wa kuchaji gari hilo nyumbani kwake.

Kwa mantiki hiyo, MO atakuwa akirudi nyumbani usiku analichaji ili asubuhi liwe limejaa kwa ajili ya mizunguko yake, lisije kumzimikia njiani.

Makadirio ya kununua Tesla Model 3, kulisafirisha mpaka nchini, kodi na kuwatela wataalamu wa kumfungia mfumo wa kuchaji gari lake nyumbani kwake, inaweza kufikia kati ya Sh250 milioni. Watekaji wote salamu zenu kutoka kwa MO. Ni salamu za kufungia mwaka 2018.