Jeuri ya Zahera kwa Zesco ipo kwa nyota hawa

Wednesday September 11 2019

 

By YOHANA CHALLE

Dar es Salaam.Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera atakuwa na kibarua kizito Jumamosi wakati atakapomvaa na George Lwandamina wa Zesco katika mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga mpaka sasa imecheza michezo 16 kuanzia Julai 15 mwaka huu na kupachika mabao 34 itakuwa na jeuri kubwa kutoka kwa wachezaji hawa walioibeba kuanzia michezo ya kirafiki hadi ile ya kimataifa.

Patrick Sibomana ndio mchezaji anayeongoza kwa kufunga mabao nane, alianza kufunga dhidi ya Tanzanite katika ushindi wa mabao 10-1 walipokuwa kambini Morogoro, akatupia tatu dhidi ya Moro Academy akafunga moja dhidi ya Kariobangi Sharks, Mlandege, Township Rollers michezo yote miwili.

Mpachika mabao mwingine anayetegemewa ni Sadney Urikhob ambaye tangu atue hapo ana mabao manne sawa na Mrisho Ngassa. Urikhob alitupia mawili kwenye mchezo dhidi ya Moro Academy huku akipiga moja kwenye mchezo dhidi ya Friends Rangers na ule wa Mlandege wakati Ngassa alipiga tatu dhidi ya Tanzanite na moja dhidi ya Mlandege katika ushindi wa mabao 4-1.

Davidi Molinga ambaye jana Jumanne alichangia timu hiyo ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Toto Africans wakati akipiga mabao mawili naye anaingia kwenye wachezaji waliozalisha mabao 34 ya Yanga mpata sasa na bao lake la kwanza lilikuwa dhidi ya Pamba FC katika Uwanja wa CCM Kirumba, wengine wenye mabao matatu ni Papy Kabamba Tshishimbi na Juma Balinya 'JB'.

Mrwanda, Issa Bigirimana mpaka sasa ana mabao mawili akianza kufungua ukurasa wake wa mabao katika mchezo dhidi ya Tanzanite waliposhinda 10-1 na lile dhidi ya Mawenzi Market, wakati Mapinduzi Balama, Feisal salum, Rapahael Daud, Paul Geodfrey, Lamine Moro, Deus Kaseke na Abdulaziz Makame wote wakiwa na bao moja kila mmoja.

Advertisement

Katika michezo 16 Yanga imepoteza michezo miwili, ule wa kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania ilipokubali mabao 2-0 ndani ya Uwanja wa Ushirika, na ule wa ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting walipolala kwa bao 1-0 Uwanja wa Uhuru.

Imeambulia sare tatu yote ya bao 1-1 ikianza na Malindi, Kariobangi Sharks katika Wiki ya Mwananchi, Township Rollers kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa kabla ya kubanwa tena na Pamba FC katika mchezo wa kirafiki.

Advertisement