Kamati mpya ya waamuzi ijue ina kazi nzito

Thursday February 20 2020

 

SHIRIKISHO la Soka la Tanzania (TFF) limefanya mabadiliko madogo kwenye Kamati ya Waamuzi kwa kuwapiga chini waliokuwapo na kuteua wapya.

Uteuzi huo umefanywa na Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuwateua Soud Abdi kuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, akisaidiwa na mwamuzi wa kimataifa wa zamani, Israel Nkongo, sambamba na Zahra Mohammed, John Kanyenye na Samwel Mpenzu.

Wajumbe hao wanachukua nafasi ya kina Salum Chama (Mwenyekiti), Joseph Mapunda (Makamu Mwenyekiti), Lesley Liunda, Nassib Mabruki na Omar Abdulkadir waliopigwa chini.

Mabadiliko hayo yamekuja kipindi ambacho kumekuwa na malalamiko mengi dhidi ya waamuzi ambao wamekuwa wakivurunda baadhi ya mechi za Ligi Kuu Bara.

Kwa mechi za hivi karibuni waamuzi wamekuwa wakifanya makosa kadhaa ambayo sio tu yamekuwa wakichefua mashabiki wa soka na pia kupungumza msisimko wa ligi hiyo.

Licha ya kwamba mara kadhaa kumekuwa na hatua zilizochukuliwa dhidi ya waamuzi waliokuwa wakivurunda, bado kuna matukio kadhaa yaliyokuwa akitokea kwenye mechi za ligi hiyo na kufanya wadau kuendelea kupigwa na butwaa.

Advertisement

Hata hivyo, pengine kwa kutambua kuwa kulikuwa na tatizo kwenye kamati iliyopita, huenda ndiko kulikofanya TFF kufanya mabadiliko hayo ambayo wadau wangependa kuona yanaleta tija katika soka la Tanzania.

Mwanaspoti kama wadau wa michezo tunaamini kilichofanywa na TFF kitaleta mabadiliko chanya yatakayokuwa na tija hasa ikizingatiwa kuwa, ligi ipo hatua ya lala salama kabla ya msimu wa 2019-2020 kufikia tamati na kutoa bingwa wa kuiwakilisha nchi.

Sio kutoa bingwa tu, lakini pia kuna timu ambazo zinapambana kuepuka kushuka daraja, hivyo ni muhimu waamuzi wakatenda haki na kuchezesha bila mushkeri ili hata timu zikianguka zisiwe na wa kulaumu na badala yake zijilaumu zenyewe.

Tunaamini mabadiliko hayo yanaweza kurekebisha tatizo lililokuwepo awali kwa waamuzi kama sio kuliondoa kabisa na mashabiki watakaoenda uwanjani kuangalia mechi wawe wanapata burudani na kufurahia viingilio vyao na sio vituko vinavyofanywa na marefa.

Tunajua yapo baadhi ya makosa yanayofanywa na waamuzi ni ya kibinadamu kabisa na wakati mwingine kushindwa kwenda na kasi ya mchezo, lakini bado kuna baadhi yao ni kama wanashindwa kutafsiri sheria za soka na hilo ndilo ambalo kamati inapaswa kuanza nalo.

Mbali na kuhakikisha wanawapiga msasa na kuwaweka sawa waamuzi, kamati hiyo pia tunadhani ina kazi ya kuhakikisha inawapanga waamuzi kuchezesha mechi hizi za lala salama kwa kuzingatia umakini, ubora na ushapu wao ili zile kelele za awali zisiendelee kupigwa.

Tunaamini kamati hiyo ambayo imeanza kazi mara moja ina kazi kubwa katika kusahihisha makosa yaliyojitokeza awali kwa waamuzi, lakini pia kuhakikisha mechi za lala salama zinachezwa bila ya kuwepo kwa vituko na maamuzi tata yatakayowatia doa waamuzi.

Advertisement