Kauli mpya ya Hamis Kilomoni kwenda kwa MO Dewji

Muktasari:

Kilomoni alitawala vyombo vya habari baada ya kugoma kutoa hati ya majengo ya Simba kwa uongozi mpya wa klabu hiyo

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Simba, Hamis Kilomoni amemuita mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji (Mo) mezani ili kuweka mambo sawa kwa maslahi ya klabu yao.

Kilomoni amekuwa akionyesha msimamo wake juu ya mfumo wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo amesema yuko tayari kukaa mezani na mwekezaji huyo ili kuweka mambo sawa kwa maslahi ya klabu yao.

"Sina tatizo na Mo, ndiyo sababu nimesema akitaka tukae mezani nitafanya hivyo, na si MO tu hata akitokea mwekezaji mwingine yoyote Simba nitakaa naye mezani kwa maslahi ya klabu.

"Hivyo kama MO atapenda aje tuzungumze, kikubwa ni mipango ya maendeleo iwe wazi na kila Mwana Simba haifahamu," alisema Kilomoni na kufafanua.

"Mabadiliko Simba ni ya watu siyo ya mtu, hivyo yanahitaji msukumo wa pamoja, japo kwenye wengi pana mengi, wengine waongo, wengine wakweli na wengine watazamaji," alisema Kilomoni.

Alisema kama MO atakuwa tayari kukaa mezani, moja ya mambo watakayozungumza naye ni msimamo wa Serikali ambao unataka klabu ya Simba kuwa na wawekezaji kuanzia watatu kuendelea ambao watagawana asilimia 49 ya hisa.

"Klabu haiwezi kuwa na mwekezaji mmoja pekee, katika asilimia 49 ya hisa, muongozo tuliopewa ni kwamba wawekezaji wasiopungua watatu watagawana asilimia 49 ya hisa na 51 zitakazobaki zitakuwa za wanachama na kila mwekezaji atakayehitaji kuwekeza Simba msimamo wa Serikali ndiyo huo," alisema Kilomoni.

Alipoulizwa kwanini yeye asimtafute MO ili wakae mezani kuweka mambo sawa kwa maslahi ya Simba, Kilomoni alisema hawezi kufanya hivyo.

"MO ni mwanangu kiumri pamoja na kwamba anataka kuwekeza Simba hivyo siwezi kumtafuta, ila akitaka tukae pamoja tuijenge Simba basi anitafute niko tayari na ninaamini tutafikia muafaka," alisema.

Afunguka kukutana na JPM

Wiki kadhaa zilizopita, picha ya Kilomoni akiwa na rais John Pombe Magufuli (JPM) zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, ambapo Kilomoni ameeleza ilivyokuwa hadi kukutana na rais.

"Rais alikuja kwenye mazishi ya mke wa kijana wangu ambaye ni Katibu Msaidizi wa CCM Zanzibar," alisema.

Alisema walipokutana walizungumza, lakini mazungumzo baina yake na rais hayamhusu mtu mwingine yoyote.

Mdhamini huyo wa Mali za Simba alisema 'fukuto' linaloendelea hivi sasa kati ya Mwenyekiti Sued Mkwabi na MO ni suala ambalo anaamini litapita kwani kikubwa ambacho Mkwabi amemueleza kimeibua sintofahamu ni kutaka mipango ya maendeleo iwe wazi.

"Ila yote hayo hakuna shaka yatapita na kila kitu kitakwenda sawa na klabu yetu itapata muafaka wa jambo hili," alisema Kilomoni.