Kobe achaguliwa kuingia Hall of Fame

New York. Gwiji wa zamani wa mpira wa kikapu katika Ligi ya Marekani (NBA), Kobe Bryant aliyefariki mwezi uliopita kwa ajali ya helkopta, amechaguliwa kuingia katika kumbukumbu za wachezaji waliofanya makubwa kwenye ligi hiyo na kuwa nje ya mchezo huo baada ya miaka mitatu na kuendelea.

Kobe ambaye alifariki Februari 26, mwaka huu pamoja na binti yake, Gianna na watu wengine saba waliokuwa pamoja, ameungana na wakali wengine waliowahi kutamba katika ligi hiyo ambao ni Kevin Garnett na Tim Duncan.

Anakumbukwa kwa kucheza misimu 20 ya ligi hiyo akiwa na Los Angeles Lakers na jezi zake namba 8 na 24 kustaafishwa baada ya kifo chake.

Bryant aliingia kwenye kikosi cha wachezaji nyota (All-Stars) mara 18 akiwa na mataji matano ya NBA ikiwamo kushikilia nafasi ya nne kwa ufungaji wa muda wote kwenye ligi hiyo.

Ukiachana na majina mengine saba ya yaliyoingia katika orodha ya mwisho ya kuingia ‘Hall of Fame’ katika hafla itakayofanyika huko Massachusetts, Agosti 29, kutegemeana na hali ya virusi vya corona itakavyokuwa, jina la Kobe huenda likawa tukio litakalombusha mambo mengi.

Garnett aliyetwaa taji la NBA akiwa na Boston Celtics mwaka 2007-2008 akiitumikia kwa muda mrefu timu ya Minnesota Timberwolves aliingia katika kikosi cha All-Stars mara 15 pamoja na mchezaji bora mwenye thamani (MVP) wa fainali, amefurahishwa kuteuliwa kuwa kwenye orodha moja na Kobe ambaye hatakuwepo siku hiyo.