Kocha wa Simba Sven afunguka sakata la Ndemla kuwindwa na Yanga

Monday April 13 2020

 

By CHARLES ABEL

HUENDA mashabiki wa Yanga wakasonya mitaani, huku wenzao wa Simba wakachekelea baada ya Kocha Sven Vanderbroeck kumaliza ubishi juu ya kiungo fundi wa mpira aliyepo kwenye kikosi cha Msimbazi, Said Ndemla anayetajwa kuwindwa Jangwani kwa mara nyingine.

Kocha Mkuu wa Wekundu wa Msimbazi, amekata mzizi wa fitina wa kufichua kutokuwepo kwa uwezekano wa Ndemla kutemwa na timu hiyo katika dirisha kubwa la usajili labda kiungo huyo aamue mwenyewe kuondoka na kutimkia kwingine.

Akizungumza wakati alipokuwa akijibu maswali ya mashabiki kupitia kurasa za Instagram, Twitter na Facebook za Simba juzi, kocha huyo kutoka Ubelgiji amedai Ndemla ni mchezaji mzuri na hana shaka na kiwango chake kama ilivyo kwa wengine ambao wamekuwa hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara.

“Ndemla ni mchezaji mzuri anayetumia mguu wa kulia. Anaweza kupiga pasi ndefu zinazofika kwa usahihi, ingawa ana changamoto ya kutokuwa na nguvu.

“Tuna idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza katika nafasi ya kiungo na anabanwa na uwepo wa wachezaji wenye manufaa makubwa.

“Kimsingi tuna kikosi kikubwa na tunachoweza kuendelea nacho kwani kila kocha anataka kila eneo liwe na wachezaji bora hivyo wachezaji waliopo wanatosha,” alisema Sven.

Advertisement

AWAKOMALIA WABRAZILI

Akijibu swali la kutowapa nafasi nyota wawili raia wa Brazil, Tairone Santos na Gerson Fraga, kocha huyo aliwasifu wachezaji hao kwa nidhamu, juhudi na uvumilivu walionao.

“Ni wachezaji wenye weledi wa hali ya juu hawalalamiki, wana furaha na wanatusaidia. Tairone amekuwa akitusaidia katika kucheza mipira ya juu pale anapopangwa na Fraga amekuwa na mchango katika safu ya kiungo,” alisema Sven.

AMVUTA KIKOTI KIAINA

Kocha huyo amefichua kwamba amekuwa akikoshwa na kiwango cha kiungo wa Namungo FC, Lucas Kikoti kutokana na aina yake ya uchezaji.

“Ukiondoa waliopo Simba, navutiwa zaidi na mchezaji anayevaa jezi namba nane (8) wa Namungo FC (Lucas Kikoti) ambaye Machi alikuwemo miongoni mwa wachezaji walioitwa katika timu ya Taifa.

“Nilimuona katika ile mechi yetu na wao. Alicheza vizuri na alifunga bao zuri baada ya kupokea vyema mpira na kujitengea kisha kupiga shuti,” alifichua kocha huyo.

AMTEGA STRAIKA MPYA

Simba inatajwa kuwa katika mipango ya kusaka mshambuliaji mmoja wa kati kusaidiana na John Bocco na Meddie Kagere lakini ikiwa atakosekana, kocha huyo amefichua kuwa kurejea kwa Miraji Athumani ni kama usajili mpya.

“Upande wa washambuliaji sifikirii zaidi ila nahitaji wachezaji wa ziada katika nafasi ya kiungo mkabaji kwa ajili ya kutengeneza balansi ya kitimu.

“Nautazama urejeo wa Miraji kama usajili mpya kwa sababu alikuwa anatoa sapoti nzuri kwa Bocco na Kagere. Kabla hajaumia, alifunga mabao sita katika mechi 10 hivyo unaweza kuona ni mchezaji wa namna gani,” alisema Sven.

Ndani ya Simba kwa sasa Jonas Mkude ndiye kiungo mkabaji tegemeo na kocha Sven amemwagia sifa na kudai anamuamini, japo anataka wa kusaidiana naye.

HATAKI UBINGWA MEZANI

Kwa sasa kumekuwa na mjadala juu ya hatima ya ligi kutokana na kusambaa kwa virusi vya corona ambapo wapo wanaoshauri msimu wa ligi ufutwe na kinara wa msimamo wa ligi apewe ubingwa na wengine wanashauri ligi iendelee tena ikiwa hali itakuwa sawa.

Kwa upande wake Sven amefichua kuwa hapendelei kuona Simba inapata ubingwa mezani na badala yake ivuje jasho uwanjani.

“Nadhani maambukizi bado hayajasambaa nchini na nahisi bado kipindi kibaya hakijaja hivyo nadhani ni vyema mechi zikachezwa wakati hali ya huu ugonjwa imekwisha uamuzi ufanyike kwa sababu za kimichezo kwa matokeo ya uwanjani. Kila timu ipate inachostahili,” alisema kocha huyo.

YANGA YAMPA AKILI

Kocha huyo anasema kuwa timu yake ilicheza vizuri mechi zote mbili msimu huu dhidi ya Yanga, ingawa ilivuna pointi moja na akafichua kuwa zimewasaidia kujifunza vitu kadhaa.

“Tumejifunza kuweka presha mapema kwa wapinzani ili kuwanyima nafasi ya kutushambulia kwa kutushtukiza,” alisema kocha huyo.

Katika mechi ya kwanza baina yao, Yanga ilichomoa mabao mawili ndani dakika na kulazimisha sare ya 2-2 kabla ya mechi ya marudiano, Vijana wa Jangwani kushinda shoo hiyo bao 1-0, shukrani kwa ile ‘frii-kiki’ tamu kutoka kwa Bernard Morrison iliyopongezwa hadi na kipa Aishi Manula.

AWAPOTEZEA TSHISHIMBI, BM33

Kocha huyo amedai kuwa kwa sasa hahitaji mchezaji yeyote kutoka katika kikosi cha Yanga kwa sababu alionao ni nyota wa daraja la juu.

“Kwa sasa simhitaji na sioni uwezekano kwa mchezaji yoyote kusajiliwa kutoka Yanga na kikosi tulichonacho kinatosheleza,” alisema Sven.

HAPENDI UGALI KAMA MASANJA

Unaukumbuka ule wimbo maarufu wa Masanja Mkandamizaji wa ‘Sitaki Ugali”, uliokuja baada ya ngoma ya Sir Juma Nature ya Ugali kubamba sana nchini enzi hizo Kibla akifunika? Basi kumbe hata Sven naye ni mmoja ya watu wasiopenda ugali buana.

Kocha huyo amefichua kwamba licha ya ugali kuwa chakula kinachopendwa hapa Tanzania, yeye amekuwa hakipendelei sana.

“Hapa chakula kinachopendwa sana ni ugali na kule Zambia unaitwa sima. Hata hivyo mimi sio mpenzi sana na napendelea zaidi vyakula vya baharini.

“Ninapokuwa mwenyewe napenda kutumia muda wangu nikiwa ‘alone’. Kusoma vitabu, kufanya mazoezi ya viungo na kukimbia na huwa sipendelei sana kuwa na watu wengi.

“Kila eneo hapa Tanzania lina vitu vyake vya upekee. Mwanza nilipapenda kwa sababu pana hali ya jua na maeneo mengine ni Morogoro na Iringa. Morogoro nilipenda kwa sababu ya mlima natamani niende kule siku moja ili nikaupande nikaone pakoje,” alisema Sven.

Advertisement