Man United yaachana na watano

Muktasari:
- Sancho aliitumikia Chelsea kwa mkopo msimu uliopita, lakini timu hiyo haikuamua kumnunua mazima kwa pauni 25 milioni zilizohitajika.
Manchester, England. Jumla ya wachezaji watano rasmi wameshapewa ujumbe wa kutafuta timu nyingine katika dirisha hili na kocha Ruben Amorim ikielezwa Jadon Sancho atakuwa ndio wakwanza kuondoka.

Mbali ya Sancho mchezaji mwingine ambaye anaweza kuondoka kwa wiki kadhaa zijazo ni winga mwenzake Antony, ambaye anadaiwa kutakiwa kurejea tena Real Betis ya La Liga.
Juventus inapambana kutaka kufanikisha makubaliano ya kumnasa Sancho, ambaye hajacheza mechi yoyote ya ushindani na Man United tangu alipopishana na aliyekuwa kocha, Erik ten Hag, miaka miwili iliyopita.

Nyota huyo wa zamani wa England mwenye umri wa miaka 25 anadaiwa kuwa na nia ya kuhamia Italia, licha ya kuhitajika pia na timu za Uturuki.
Sancho aliitumikia Chelsea kwa mkopo msimu uliopita, lakini timu hiyo haikuamua kumnunua mazima kwa pauni 25 milioni zilizohitajika.
Man United bado inataka dau kama hilo ikiwa timu yoyote inamhitaji kiasi ambacho sio kikubwa sana lakini changamoto inaonekana kuwa katika mshahara kani Sancho anahitaji pauni 7 milioni kwa mwaka.
Sancho amekuwa na kipindi kigumu katika miaka minne ndani ya Old Trafford tangu aliposajiliwa kwa dau la pauni 73 milioni kutoka Borussia Dortmund mwaka 2021.

Kwa upande mwingine, Real Betis wanatarajia kufikia makubaliano ya kumrejesha Antony baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa kwa mkopo.
Mchezaji huyo kutoka Brazil mwenye umri wa miaka 25 amekuwa na maisha mazuri Hispania msimu uliopita na pia alikaa huko wakati wa mapumziko ya msimu.
Hadi sasa, hakuna timu nyingi zilivyoonyesha nia ya kumnasa Antony, jambo linalowapa matumaini Manuel Pellegrini na Betis yake kuwa watampata.

Mbali ya hawa, mastaa wengine ambao Amorim anadaiwa kuwa ameshawasiliana nao ni Marcus Rashford, Alejandro Garnacho, na Tyrell Malacia ambao pia wapo katika mpango wa kujiunga na timu nyingine tayari.