Rashford atinga mazoezini United licha ya kuelezwa akae pembeni

Muktasari:
- Rashford alikuwa na mgogoro na kocha Ruben Amorim, kabla ya kupelekwa kwa mkopo Aston Villa.
Manchester, England. Marcus Rashford ameripoti mazoezini katika kituo cha Carrington mapema wiki hii licha ya kuwa miongoni mwa wachezaji watano wa Manchester United waliopaswa kukaa mbali na kikosi hicho ili kukamilisha mipango ya kuondoka klabuni hapo.

Rashford, mwenye umri wa miaka 27, anaripotiwa kurejea Jumatatu na Jumanne, ingawa hakuungana na wachezaji wenzake kwenye mazoezi ya timu bali alifanya programu ya mazoezi binafsi.
Nyota huyo wa Kimataifa wa England anatajwa kuhusishwa na klabu za Barcelona na Bayern Munich, huku jezi yake namba 10 tayari ikikabidhiwa kwa Matheus Cunha ambaye amesajiliwa kutokea Wolverhampton.
Mbali na Rashford, wachezaji wengine waliopaswa kutokuwepo kambini ili kutafuta timu mpya ni Alejandro Garnacho, Antony, Jadon Sancho na Tyrell Malacia. Hata hivyo, wote bado wanaruhusiwa kutumia huduma za kitabibu na sehemu za mazoezi katika kituo cha Carrington au kwa njia ya mtandao.
Hatua hiyo ya klabu inalenga kuepuka kuvunja mikataba ya wachezaji hao, kwa kuwapa muda wa kutosha kupanga mustakabali wao huku wakipata huduma zote muhimu kiafya.

Rashford anadaiwa alikuwa na mgogoro na kocha wa United, Ruben Amorim, kabla ya kupelekwa kwa mkopo Aston Villa katika nusu ya pili ya msimu uliopita. Hata hivyo, taarifa za ndani zinaeleza kuwa mchezaji huyo alikuwa na nia ya kushiriki maandalizi ya msimu mpya kwa asilimia 100.
Kwa sasa, United wanakaribia kukamilisha usajili wa Bryan Mbeumo kutoka Brentford, lakini inaripotiwa kuwa watahitaji kuuza baadhi ya wachezaji wao ili kufanikisha usajili zaidi katika dirisha hili la majira ya joto.
Ratiba ya mechi za maandalizi kwa msimu mpya kwa Red Devils inatarajiwa kuanza Julai 19 kwa mchezo dhidi ya Leeds utakaopigwa jijini Stockholm, kabla ya kuelekea Marekani kwa maandalizi mengine.