Rashford apokwa jezi Man United

Manchester, England. Staa wa Manchester United, Marcus Rashford amevuliwa jezi yenye namba 10 na timu yake na kupewa staa mpya Matheus Cunha.
Man United imesema kwamba Rashford ni miongoni mwa mastaa watano wa kikosi cha kwanza ambao wameiambia klabu wanataka kuhama kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.
Cunha amekabidhiwa jezi huyo Namba 10, ambayo iliwahi kuvaliwa na wachezaji magwiji kwenye kikosi hicho chenye maskani yake Old Trafford.
Cunha, ambaye ni usajili wa kwanza wa Man United kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi wakati saini yake iliponaswa kwa Pauni 62.5 milioni akitokea Wolves, alikuwa akiitolea macho jezi Namba 10 kabla ya kujiunga na miamba hiyo.
Staa huyo ambaye ni raia wa Brazil mwenye miaka 26, anaamini atarudisha yale makali ya Wayne Rooney kwenye klabu hiyo. Baadhi ya wachezaji mahiri kabisa wa Man United walivaa jezi Namba 10, hivyo kufanya jambo hilo kuwa na maana na presha kubwa kwa wachezaji.
Kwenye kikosi cha Man United, Rashford amevaa namba tatu tofauti, 39, 19, na 10 - huku Namba 10 alikabidhiwa mwaka 2018. Lakini, uamuzi wa kocha Ruben Amorim umebainisha kwamba baada ya ujio wa staa mpya kwenye kikosi chake, hivyo Rashford hana nafasi tena.
Katika zama za Ligi Kuu England, kuna wachezaji 10 walivaa jezi Namba 10. Kabla ya 1993, wachezaji waliokuwa wamevaa jezi hiyo ni George Best, Sir Bobby Charlton na Denis Law, ambapo kipindi hicho pia namba zilikuwa zinavaliwa tu hovyohovyo, hakuna mchezaji mwenye namba yake.
Rashford anaondoka United akiwa ameichezea michezo 443 na kufunga mabao 142 akiwa amekaa hapo kwa misimu 10.