Kocha wa Yanga Eymael sasa kusajili wachezaji 10 wapya

KOCHA wa Yanga, Luc Eymael yuko mapumzikoni nchini Ubelgiji. Lakini amezungumza na Mwananchi Digital na kuweka wazi kwamba mpaka sasa ana majina ya wachezaji wapya zaidi ya 10 mkononi.

Amesisitiza kwamba katika orodha hiyo wamo wachezaji wa ndani na nje ya Tanzania na inaweza kuongezeka kwavile hajafanya uamuzi wa mwisho amchukue nani au ampige chini nani.

Lakini akasisitiza kwamba kwa ajili ya msimu msimu ujao inakuja Yanga ya sura tofauti kabisa na anachofanya sasa ni kuwaongeza mikataba wachezaji wote muhimu anaotaka kubaki nao kwa kuanzia na wale waliocheza muda mrefu na kwamba viongozi wameshafikia pazuri kwavile wanamwambia kila kitu na hata kopi za mikataba wanamuonyesha.

Kocha huyo amesisitiza kwamba orodha hiyo hata baadhi ya viongozi hawaijui kwavile bado ni siri yake na benchi lake la ufundi ingawa nao pia siyo wote wanaoijua.

“Tunajaribu kuangalia na kufuatilia wachezaji wazuri wakati huu ili muda muafaka ukifika tusipate shida. Kwa maana hiyo nimekuwa na majina ya wachezaji wengi kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika ambao nimekuwa nikiwafatilia.

“Siwezi kuyataja majina hayo wakati huu kwavile wengine bado wapo kwenye mikataba na timu zao, na pia tunaweza kuwataja wakati huu ikawa mbaya kwetu kwa timu nyingine zenye nguvu ya kifedha kwenda kuwapa ofa bora zaidi yetu na wakaenda huko. Pia hatuyataji kwa sababu inaweza kufika wakati ukapata mbadala bora zaidi ya yule uliyemtaja awali,” alisema kocha huyo ambaye hawezi kurudi Tanzania kwa sasa kutokana na mipaka ya nchi yake kufungwa kutokana na janga la kusambaa kwa virusi vya corona.

“Mashabiki wa Yanga watulie msimu huu tutafanya usajili wa wachezaji wengi bora kuliko na misimu mingi nyuma iliyopita,” aliongezea Eymael ambaye amewahi kufundisha soka DR Congo, Afrika Kusini na Sudan.

Wiki hii kwenye moja ya matoleo ya Mwanaspoti, kiongozi mmoja wa Yanga alidokeza kwamba miongoni mwa wachezaji wanaowafuatilia ni kipa Jonathan Nahimana na beki wa kulia Kelvin Kajiri wote kutokea KMC. Vipo pia vichwa kutoka klabu za Namungo na Alliance.