Liverpool yaamua kupanua zaidi uwanja wake wa Anfield

Muktasari:

  • Mabingwa hao wa Ulaya wanataka uwanja huo uweze kubeba mashabiki 61,000.

Liverpool, England. Liverpool imeweka hadharani mpango wake wa kuupanua uwanja wake wa Anfield kuwa mkubwa zaidi ya ilivyopangwa.
Klabu hiyo ya Merseyside imetoa taarifa leo Alhamisi ikithibitisha kuwa wataachia maombi yao ya awali wa kupanua uwanja kuelekea jukwaa la Anfield Road kwa kuwa wanafanyia kazi mpangho mpya wa kuongeza uwezo wa kuchukua idadi kubwa ya watu.
Badala yake, watawasilisha maombi ya mpango mpya kwa ajili ya "mradi mkubwa zaidi" kwa kuwa hawaamini tena kama ongezeko la viti 4,600 ni muhimu.
Ofisa mwendeshaji mkuu wa Liverpool, Andy Hughes, alielezea hali hiyo kwa taarifa fupi.
“Maendeleo yaliyofanyika katika upembuzi yakinifu yametufanya tuwe katika nafasi inayoturuhusu kuachia maombi ya mpango wa awali,” alisema Hughes. “Tuko tayari kushirikiana na wananchi wa maeneo jirani, maofisa mipango ardhi na wengine kwa kuwa sasa tumeelekeza macho katika mapendekezo yoyote ya kuendeleza zaidi Anfield Road. Wakati wote wa mchakato huu tumeweka bayana kuwa lengo letu ni kupata suluhisho bora linaloiwezekana kwa ajili ya Anfield Road na hilo ndio linabakia kuwa suala letu.”
Awali, ofisa mtendaji mkuu, Peter Moore alisema kuwa mpango wa Liverpool kupanua jukwaa la Anfield Road kwa zaidi ya mashabiki 4,600 hautoshelezi mipango yao na kwamba uwezekano wa kufikisha idadi ya mashabiki 61,000 sasa umekaribia mahitaji yao.
Kwa sasa uwanja wa Anfield una uwezo wa kuchukua mashabiki 54,074 na ni West Ham, Tottenham, Arsenal, Man City na Man United wana viwanja vyenye uwezo wa kuchukua watu wengi zaidi kwenye Ligi Kuu.