MWAKINYO; Marefa ngumi za baa wanasema kabebwa

Sunday December 1 2019

 

By Luqman Maloto

BONDIA Hassan Mwakinyo amempiga mpizani wake, Mfilipino Arnel Tinampay kwa “majority decision’. Ndio, boxing ina ushindi wa aina tano; Knock-Out (KO), Technical Knock-Out (TKO), Unanimous Decision, Split Decision na Majority Decision.

KO ni ushindi wa bondia kumzimisha mpinzani wake na kuhesabiwa bila kinyanyuka ndani ya sekunde 10. Bondia anapoamua kutoendelea na raundi inayofuafa huitwa Retired (RTD) lakini huhesabiwa KO.

TKO ni refa anaposimamisha pambano kumwokoa bondia aliyezidiwa, au bondia mmoja anapoangushwa mara tatu ndani ya raundi moja, vilevile mkufunzi wa bondia kurusha taulo ulingoni (kusalimu amri).

Unanimous Decision ni ushindi wa majaji wote watatu. Split Decision ni ushindi wa majaji wawili dhidi ya mmoja aliyempa ushindi aliyeshindwa. Majority Decision ni ushindi wa majaji wawili dhidi ya mmoja aliyeamua droo.

Majaji wawili waliamua Mwakinyo alishinda, mmoja aliona pambano lilikuwa sare. Hivyo, Mtanzania Mwakinyo alishinda kwa “majority” katika pambano la raundi 10, uzani wa kilogramu 70, yaani super welterweight, lililofanyika Ijumaa iliyopita, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Baada ya pambano mitandaoni kumekuwa na majaji wengi ambao wanakosoa ushindi wa Mwakinyo. Wanadai kapendelewa. Ila sio mbaya, ni macho ya majaji wa ngumi za baa, huwezi kuyalaumu.

Advertisement

Ngumi za baa walevi wanapopigana kila konde huhesabiwa hata kama lilizuiwa kutua. Makonde ya tumbo hupewa pointi zote. Tena kuna mlevi anaweza kujisifu “mliona nilivyompa za tumbo?”

Ngumi za kwenye vilabu vya pombe hata anayemlalia mwenzake huhesabiwa. Makonzi na makofi pia. Boxing ina kanuni zake. Boxing sio kickboxing wala martial arts.

Kuna watu wamefikia hatua ya kusema kuwa katika boxing ukipigana ugenini inabidi ushinde kwa KO, kwa pointi lazima mwenyeji apewe ushindi.

Wanakumbusha Fight of the Century la Floyd Mayweather jr dhidi ya Manny Pacquiao. Eti, Pacquiao alimwadhibu Mayweather lakini alinyimwa ushindi.

Wanasahau kuwa wataalam wote wa boxing walisema Mayweather alishinda kwa sababu alitua jabs zenye akili usoni kwa Pacquiao ambaye alikuwa anarusha ngumi nyingi zisizo na pointi.

Mike Tyson ambaye kabla ya pambano alimpa ushindi Pacquiao, baada ya mchezo alisema, Pacquiao hakupigana kwa akili na alirusha ngumi nyingi zisizo na faida.

TUCHUKUE HAPO!

Kutoka kwa Tyson tunapata kitu kuwa kwenye boxing kuna kupigana na kupigana kwa akili. Na ieleweke kuwa anayepigana kwa akili ndiye hushinda, maana hujua wakati gani ajilinde, afanye mashambulizi ya kushitukiza au ya nguvu. Na wapi apige kupata pointi.

Majaji katika boxing huhesabu pointi raundi kwa raundi. Na kila raundi huwa na alama 10 kwa anayeongoza, na tisa kwa aliyepoteza raundi, hivyo wastani wa kila raundi huwa 10-9.

Bondia anapoangushwa hupoteza pointi moja, mara mbili pointi mbili. Na anayecheza faulo hupoteza pointi. Hutokea pia jaji kuamua kumpa bondia ushindi wa pointi 10-8 hata kama hajamwangusha mwenzake ulingoni. Ni pale anapoona mshindi wa raundi ametawala mchezo kwa kiasi kikubwa.

Katika pambano la raundi 10 ambalo Mwakinyo alipigana, maana yake lilikuwa na pointi 100 kwa kila bondia. Yaani pointi 10 mara raundi 10. Hutegemea kila raundi bondia atavuna nini.

Kama bondia anashinda raundi 6, maana yake ana pointi 10 mara sita, jumla pointi 60. Na anakuwa ameshindwa raundi nne, kwa hiyo alama tisa mara raundi nne ni 36. 60+36=96.

Bondia aliyeshindwa raundi sita na kushinda nne, maana yake anahesabiwa pointi 10 kwa kila raundi aliyoshinda, hivyo 10 mara nne ni 40. Kisha alama tisa kwa kila raundi aliyopoteza, hivyo unakokotoa 9 mara 6, unapata 54. 40+54=94. Ni hapo jaji anaweza kuibuka na matokeo ya pointi 96-94.

Jaji mwingine kwa jicho lake hutoa pointi na kufanya majumuisho. Kuna raundi jaji mmoja anaweza kutoa pointi 10-9, mwingine akaona ni 10-10, kwamba mabondia wote walilingana alama. Vilevile yupo jaji anaweza kutoa 10-8. Macho ya majaji watatu ndio huamua mshindi ni nani au droo baada ya raundi kukamilika.

Hapo maana yake ni kuwa katika boxing ushindi wa kila raundi una maana kubwa. Sio unaruhusu ngumi nyingi katika raundi nyingi, halafu pambano likiwa linaelekea ukingoni ndio unaamka na kushambulia kwa nguvu.

Kama umeshapoteza raundi 7, kisha ukaamka raundi tatu za mwisho. Ikiwa hesabu ya jaji itakupendelea alama tisa kwa kila raindi maana yake utapata 63 katika raundi 7 na 30 kwenye raundi tatu ulizoshinda. Jumla ni pointi 93.

Mpinzani wako ambaye alishinda raundi 7 atapata pointi 70 na tatu ulizomshinda, atapata 27. Jumla 97. Hivyo matokeo ya jaji yataonesha 97-93. Umeshindwa!

Kanuni ya boxing ni kushinda kwa KO au kuongoza raundi nyingi. Anayepoteza raundi nyingi ni vigumu kutarajia miujiza ya kushinda pambano.

MACHO YA MAJAJI

Nini ambacho majaji huangalia katika kutoa pointi kwenye boxing? Hili ndilo eneo ambalo wengi wakilifahamu, pengine litapunguza kelele za majaji wa ngumi za baa na vilabu vya pombe.

Boxing ni taaluma. Majaji ambao huketi kuusoma mchezo, kuutafsiri na kuamua pointi za raundi kwa raundi kwa kila bondia, ni taaluma yao. Hujua nini ambacho mchezo wa ngumi unahitaji kupata mshindi. Na hufahamu kuwa boxing ni tofauti na martial arts.

Mosi majaji huangalia mashambulizi yenye macho (effective aggression). Mashambulizi huwafanya majaji kumwona mtawala wa raundi. Hivyo ni muhimu kushambulia.

Hata hivyo, unaweza kurusha makonde ya hovyohovyo ambayo hayatahesabiwa. Kwa maana inabidi ufanye mashambulizi yenye macho kusudi ngumi zako zifike maeneo ambayo yatafanya uhesabiwe pointi.

Bondia anayefanya mchezo uende kulingana na matakwa yake au mtindo wake kupigana ulingoni (ring generalship), humshawishi jaji kumpa alama za kuongoza raundi kwa raundi.

Ulinzi (defense). Bondia anajilinda vipi dhidi ya mpinzani wake? Aina ya ulinzi pia humshawishi jaji. Kwamba bondia anaweza kushambuliwa sana, lakini uwezo wake wa kujilinda na kumkimbia mpinzani ulingoni, humfanya jaji ampe pointi.

Makonde mazito yenye kutua waziwazi (hard and clean punches). Hapa ndipo wengi huchanganywa. Makonde mengi ambayo hayaonekani kutua waziwazi kwa mpinzani ni kujichosha. Majaji hushawishiwa na makonde mazito yenye kutua dhahiri kwa mpinzani.

Hata kama ni jab nyepesi lakini inayoonekana vizuri, humshawishi jaji. Na hiyo ndio siri ya ushindi wa Mwakinyo kwa Tinampay. Majaji wa ngumi za baa ni vigumu kuuona ushindi wa Mwakinyo.

Wanashindwa kuelewa kuwa Mwakinyo alichukua pointi kwenye raundi nyingi na Tinampay aliamka raundi za mwisho. Na Tinampay alikuwa anapiga ngumi za baa, Mwakinyo alirusha makonde ya ulingoni na kichukua pointi.

Pamoja na ushindi, yapo maeneo Mwakinyo anahitaji kufanyia kazi. Aongeze mazoezi ya uvumilivu, raundi mbili za mwisho alionekana kuchoka na kupotea. Umakini na mkazo katika kushambulia ni muhimu. Mwanzoni Mwakinyo alipompiga ngumi za tumbo Tinampay, alionekana kumwathiri.

Dhahiri Tinampay ana udhaifu mkubwa tumboni. Mwakinyo angeweza kuongeza mkazo wa kumpiga tumboni ili kumpa maumivu, apoteze umakini wa kujilinda usoni, pengine angemaliza pambano mapema au angemfanya ajilinde zaidi bila kushambulia. Ingekuwa nafasi ya Mwakinyo kutawala pambano mwanzo mwisho.

Hata hivyo, muda ulipomwenda Mwakinyo alicha kabisa kumpiga Tinampay tumboni, akamfanya apumue na kupanga mashambulizi. Mwakinyo hakutumia ipasavyo udhaifu wa tumbo la Tinampay. Kikubwa, Mwakinyo bado ni bondia mzuri, aongeze juhudi. Atafika mbali. Umri unamruhusu.

Advertisement