VIDEO: Mahakama yatupilia mbali pingamizi la Wambura

Thursday February 14 2019

By Hadija Jumanne

Dar Es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetupilia mbali na pingamizi lililowasilisha na upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura.

Wambura alifikishwa Kisutu kwa mara ya kwanza, Jumatatu Februari 11, mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha zaidi ya Sh 100milioni.

Siku hiyo baada ya Wambura kusomewa mashtaka yake, hakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokiwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Kutokana na hali hiyo, Wakili wake Majura Magafu aliwasilisha pingamizi Mahakamani hapo, akiiomba mahakama hiyo kutupilia mbali kesi hiyo kwa sababu mashtaka yote 17, hayajafunguliwa chini ya sheria ya uhujumi uchumi.

Magafu alidai kuwa kesi hiyo ilipaswa kufunguliwa kama kesi ya kawaida ya jinai ambayo inamruhusu mshtakiwa kujibu mashtaka yake.

Pia, Majura alidai kuwa katika maudhui ya hati ya mashtaka hakuna hata kosa moja la uhujumu uchumi kama ilivyoainishwa.

Magafu alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 129 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinaipa Mamlaka Mahakama hiyo kukataa kusajili kesi, endapo zina makosa, pia kupitia kifungu hicho kinaipa mamlaka mahakama husika kuikataa na kuitupilia mbali kesi husika.

Akitoa uamuzi huo, leo Alhamisi Februari 14, 2019, baada ya kupitia hoja za pande zote, Hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina alisema, kifungu cha 3 cha Sheria ta Uhujumu Uchumi, kinaondoa Mamlaka ya Mahakama ya Kisutu, kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi, isipokuwa DPP atakapowasilisha kibali cha kuiruhusu mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo.

Mhina amesema Mahakama ya Kisutu, ina  Mamlaka ya kumsomea mshtakiwa mashtaka yake pamoja na maelezo ya Mashahidi na Vielelezo (Committal Proceedings) na sio vinginevyo.

"Mahakaka ya Kisutu imefungwa mikono, haina Mamlaka ya kuondoa au kufanya maamuzi yoyote katika hati hii ya mashtaka, mpaka itakapopata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) cha kuruhusu kesi hii kusikilizwa hapa" amesema Hakimu Mhina na kuongeza

"Hivyo mahakama hii haina Mamlaka ya kuondoa kesi  na kwamba masuala ya kisheria yaliyowasilishwa na upande wa utetezi, yanatakiwa kuelekezwa katika Mahakama yenye Mamlaka ambayo ni Mahakama Kuu" amesema Hakimu Mhina na kuongeza

Hakimu Mhina baada ya kueleza hayo, alisema upande wa utetezi kama hawajaridhika na uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kisutu, wanaweza kupata rufaa Mahakama Kuu.

Hakimu Mhina, baada ya kutoa maamuzi hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi, Februari 28, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutoka na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana.

Wambura anakabiliwa na mashtaka hayo 17 katika kesi ya Uhujumu uchumi namba 10/2019.

Katika mashtaka hayo 17 yanayomkabili Wambura; shtaka moja ni la kughushi, shtaka moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo; mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Advertisement