Man City waifikia rekodi ya miaka 126

Wednesday December 5 2018

 

London, England. Ikicheza ugenini jana Manchester City iliifunga Watford mabao 2-1, na kufikia rekodi ya miaka 126, mbali ya kuzidi kuongoza Ligi Kuu England.

Mabao ya washindi hapo jana yalifungwa na Leroy Sane dakika ya 40 na Riyad Mahrez 51 na nile la Watford likafungwa na Abdoulaye Doucoure dakika ya 85.

Man City imekuwa timu ya kwanza kushinda mechi 11 mfululizo za Ligi kwa mabao kuanzia mawili na kuendelea wakati kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola, kikiendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo katika Ligi Kuu England msimu huu.

Ikiwa imecheza mechi 15 Man City imefunga mabao 45 na kufungwa saba ikiwa na wastani wa mabao 38 idadi kubwa ambayo haijawahi kufikiwa kwa miaka 126 iliyopita.

Timu ya mwisho kuwa na uwino mkubwa wa mabao nchini Uingereza baada ya kucheza mechi 15 ni Sunderland rekodi iliyoweka msimu wa mwaka 1892-93 ilipofikisha wastani wa mabao 38 kabla ya mapumziko na mwisho wa mchezo huo wa 15 ikafikisha 39.

Aidha Man City imefunga kuanzia mabao mawili katika kila mchezo waliocheza na Watford katika mechi tisa za mwisho ikifunga mabao 29 na kufungwa matano.

Nayo Watford kwa mara ya kwanza tangu imekuwa chini ya kocha Javi Gracia imepoteza mechi tatu mfululizo za Ligi mara ya mwisho kupata vipigo mfululizo ilikuwa Desemba 2017 wakati huo ikiwa chini ya kocha aliyetimuliwa Marco Silva.

Ukijumulisha na mechi za mwisho wa Ligi ya msimu uliopita, Man City haijapoteza katika michezo michezo 21, kipigo chao cha mwisho kilikuwa cha mabao 3-2 walichokipata kutoka kwa Man United, Aprili mwaka huu.

Winga Riyad Mahrez amekuwa ndiye mchezaji wa Man City aliyeifunga zaidi Watford tangu akiwa Leicester City hadi sasa ameifunga mabao sita katika Ligi Kuu pekee.

 

Advertisement