Manchester United yamtoa mafichoni Van der Sar

Muktasari:
Nguli huyo alitwaa mataji manne ya Ligi Kuu England tangu aliposajiliwa akitokea Fulham.
London, England. Kipa nguli wa zamani wa Uholanzi, Edwin Van der Sar ametoa kauli nzito kwa klabu yake ya zamani Manchester United kutokana na mwenendo mbaya msimu huu.
Nguli huyo alisema wachezaji wa Man United wamepoteza mfumo wao hali inayochangia timu hiyo kuyumba.
Van der Sar anakumbuka namna Man United ilivyokuwa na nguvu enzi zao ikiwa chini ya akina Roy Keane, Gary Neville, Paul Scholes na Rio Ferdinand.
Kocha Ole Gunnar Solskjaer yuko kikaangoni baada ya kupata matokeo mabaya msimu huu. Man United ina pointi tisa na ipo nafasi ya 12 katika msimamo.
Kipigo cha bao 1-0 ilichopata Newcastle United Jumapili kimemuibua nyota huyo aliyecheza kwa mafanikio Old Trafford.
“Nadhani wanapaswa kujitathimini, wakati ule mkiwa ndani ya vyumba vya kuvalia nguo utakutana na akina Ryan Giggs,”alisema nguli huyo aliyecheza miaka sita Man.
Van der Sar alisema kila mchezaji anapaswa kujiona ni sehemu ya Man United, lakini hali ni tofauti kwa wachezaji wa sasa aliodai hawachezi kwa mapenzi ya klabu. Nguli huyo alitwaa mataji manne ya Ligi Kuu tangu aliposajiliwa akitokea Fulham.