VIDEO: Manula afunguka ugomvi na Tshabalala

Dar es Salaam. Kipa wa Simba, Aishi Manula amesema kilichotokea baina yake na beki wa kushoto wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kwenye mechi waliyolala 1-0 dhidi ya Kagera Sugar juzi Ijumaa kiliishia kwenye Uwanja wa Uhuru ilipochezwa mechi hiyo.

Manula na Tshabalala walionekana kutunishiana vifua baada ya beki huyo wa kushoto kujifunga goli kizembe akimnyima nafasi kipa huyo ambaye alionekana akienda kuudaka kirahisi mpira na kuipa Simba kipigo cha tatu mfululizo kutoka kwa timu hiyo ya Kagera.

Manula alidai kuumizwa na kilichotokea hivyo alishindwa kujizuia na hatimaye kutokea kilichotokea, lakini watu wasimchukulie vibaya kwa sababu yeye na Tshabalala ni marafiki.

“Tshabalala ni rafiki yangu tena wa karibu, yalitokea uwanjani yameishia palepale, lile tukio lilichangiwa na damu kuchemka, sipendi kuliongelea kiundani zaidi ila ifahamike kuwa sina ugomvi wowote naye,” alisema Manula.

Kagera Sugar imechukua pointi zote sita kutoka kwa vinara hao wa Ligi Kuu ya Bara msimu huu baada ya pia kuilaza Simba 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba Aprili 14.