Mashabiki wa Spurs waliomrushia ndizi Aubameyang wajuta

Muktasari:

  • Mashabiki wa timu ya Tottenham Hotspurs waliomfanyia vitendo vya kibaguzi mshambuliaji wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang, wamejutia vitendo vyao na sasa wanatarajiwa kupandishwa kizimbani Desemba 31 mwaka huu katika Mahakama ya Highbury Corner.

London, England. Mashabiki wanazi wa timu ya Tottenham Spurs waliomdhihaki kwa kumrushia ganda la ndizi mshambuliaji wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang, wameomba radhi wakijutia vitendo vyao.

Aubameyang alikumbwa na kadhia hiyo wakati akishangilia bao la kuongoza la Arsenal alilofunga katika mchezo wa mahasimu wa jiji la London Kaskazini dhidi ya Tottenham, walioshinda kwa 4-2.

Mmoja wa manazi hao Averof Panteli, 57, aliapa mbele ya Kamati ya maadili ya Chama cha Soka England (FA) akisema hana chembe za kibaguzi bali alifanya kosa hilo kwa mhemko wa kimichezo.

Mzaliwa huyo wa London, Kaskazini anayeishi Mjini Norwich na wenzake wawili walikula kiapo kilichokubaliwa na FA ikerishidhia baada ya rekodi zao kuonyesha hawana tabia hiyo hivyo kuwafutia mashitaka ya kibaguzi lakini watapambanda kizimbani katika Mahakama ya Highbury Corner Magistrates, Desemba 31 mwaka huu.

“Ninaapa kuwa mimi sio mbaguzi kabisa na wala sijawahi kufikiria mambo ya kibaguzi, ninaomba hata muwaulize watu walio karibu na mimi ama muangalie rekodi zangu mimi sina tabia ya ubaguzi hata kidogo nilipitiwa tu ninaomba msamaha,” alisema Panteli.

Shabiki huyo aliwaomba radhi mashabiki wa Arsenal na wale wa klabu yake ya Tottenham kwa kuwaaibisha akisema hakutarajia hata siku moja kama ingetokea akafanya jambo la kufedhehesha hadharani.

Wengi wa mashabiki wa soka barani Ulaya wamekuwa wakiendeleza vitendo vya ubaguzi wa rangi licha ya juhudi kubwa inayofanywa na Fifa na Shirikisho la soka Ulaya (Uefa), kupiga vita ubaguzi.