Mashabiki wamkataa Neymar PSG

Monday August 12 2019

 

Paris, Ufafansa. Mashabiki wa Paris Saint-Germain wamemtolea uvivu mshambuliaji Neymar katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Ufaransa iliyochezwa jana.

Licha ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Nimes, mashabiki wa PSG walikwenda uwanjani na mabango ya kumtaka Neymar kuondoka ndani ya klabu hiyo.

Neymar ameibua mzozo wa muda mrefu na klabu yake akishinikiza kuondoka katika usajili wa majira ya kiangazi.

Miamba ya soka Hispania Barcelona na Real Madrid, inahusishwa na mpango wa kumsajili nahodha huyo wa zamani wa Brazil.

Mbali na kwenda mabango, mashabiki hao walipaza sauti wakitaka PSG kuharakisha uhamisho wa Neymar kwa kuwa hawamtaki.

Mashabiki wa PSG hawaoni mchango wa Neymar kama Kylian Mbappe, Edinson Cavani na Angel Di Maria ambao wamekuwa wafungaji wa timu hiyo katika mechi za mashindano.

Advertisement

“Neymar ondoka”. Hayo yalikuwa ni baadhi ya mabango yaliyosomeka uwanjani katika mechi hiyo ambayo PSG ilipata mabao yake kupitia kwa Mbappe, Cavani na Di Maria.

Hata hivyo Kocha wa PSG, Thomas Tuchel alisema hawezi kupata usingizi endapo Neymar ataondoka kwa kuwa ni vigumu kupata mchezaji wa kuziba pengo lake.

Advertisement