Masoud, Omog wataka kazi Yanga

Muktasari:

  • Masoud ambaye alisitishiwa mkataba na Simba mwishoni mwa mwaka jana baada ya kutofautiana na Kocha Patrick Aussems na kurejea Rwanda kukinoa kikosi cha As Kigali, ameshatimuliwa kitambo.

SIKU chache tu baada ya mabosi wa Yanga kumpiga chini Kocha Mwinyi Zahera, tayari nafasi ya Mkongo huyo Jangwani imeanza kumezewa mate kwani waliowahi kuwa makocha wa Simba, Joseph Omog na Masoud Juma wamesisitiza wanaitaka ajira hiyo ili wawape raha Wanayanga.

Kwa muda tofauti, makocha hao wamelipigia simu Mwanaspoti na kuulizia juu ya namna ya mchakato wa kuomba kazi Yanga ulivyo, ili nao waiombe kwa madai wanatamani kurejea Tanzania na kuinoa timu hiyo wakiitaja ni timu kubwa kama ilivyokuwa kwa Simba waliyoinoa kwa pamoja.

Masoud ambaye alisitishiwa mkataba na Simba mwishoni mwa mwaka jana baada ya kutofautiana na Kocha Patrick Aussems na kurejea Rwanda kukinoa kikosi cha As Kigali, ameshatimuliwa kitambo.

“Nimesikia Zahera ametimuliwa Yanga, ningependa kuja kuinoa kwani ni timu kubwa kama Simba na presha zake nazimudu, ila sijajua kwa sasa mchakato upoje, ebu nisaidie mawasiliano na watu wa Yanga,” alisema Masoud, raia wa Burundi ambaye alipokuwa Msimbazi alikuwa kipenzi cha mashabiki wa klabu hiyo, ingawa viongozi walimchomoa kwa shinikizo la Aussems.

Naye Mcameroon, Joseph Omog aliyewahi kuinoa Azam kabla ya kurejea kuifundisha Simba iliyomfurusha misimu miwili iliyopita kutokana na kipigo na kung’olewa na Green Warriors katika mechi za Kombe la FA anaitaka ajira Jangwani.

Omog aliyewahi kuipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika 2012 AC Leopards ya Congo Brazzaville alisema: “Natamani kurejea kufundisha Tanzania, nikiamini Yanga haina tofauti kubwa na Simba, hivyo kile nilichokifanya nikiwa huko kuanzia Azam mpaka Simba nitaweza kuboresha zaidi nikiwa Yanga, ila sijajua kama tayari wameshatangaza ajira.”

Kocha huyo alisema kwa uzoefu wake wa soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla, hadhani kama atashindwa kuibeba Yanga, akisisitiza huenda akatuma wasifu wake ajira ya kuziba nafasi ya Zahera ikitangazwa.

Kwa mujibu wa mabosi wa Yanga mchakato wa kusaka kocha mkuu mpya bado haujaanza kwa vile walikuwa na kazi ya kushughulikia mechi yao ya jana dhidi ya Ndanda FC, japo walimpa kocha Boniface Mkwasa wiki mbili kabla ya kumleta kocha mkuu mpya wa kudumu kuziba nafasi ya Zahera.