Mastaa Man City wapokewa kifalme

Tuesday May 14 2019

 

London, England. Maelfu ya mashabiki wamewapa mapokezi kabambe wachezaji wa Manchester City, baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England.

Man City juzi ilitwaa ubingwa huo kwa mara ya pili mfululizo, baada ya kuichapa Brighton mabao 4-1.

Mashabiki wa klabu hiyo walijitokeza kwa wingi kuwalaki wachezaji wa Man City kwenye uwanja wao wa Etihad.

Wachezaji, viongozi na maofisa wa klabu hiyo waliwasili katika mji wa Manchester na kupata mapokezi ya aina yake kutokana na mafanikio hayo.

Mashabiki waliovaa jezi za timu hiyo walishangilia baada ya nohodha Vincent Kompany kunyanyua kombe hilo. “Hii ni mara ya pili kutwaa ubingwa katika mazingira magumu kama haya, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2012 tulipata ushindi dakika ya mwisho,” alisema Kompany.

Beki huyo alisema ushindi huo ni alama nzuri kwa Man City kwa kuwa muda wote imekuwa katika kiwango bora katika mashindano.

Riyad Mahrez alisema ilikuwa ligi ngumu na kila mmoja alipambana kuipa mafanikio Man City na haikujalisha alicheza mechi ngapi.

Raheem Sterling alisema siku zote kocha Pep Guardiola amekuwa na mtazamo chanya ambao umekuwa ukimpa mafanikio.

Kocha wa Man City Pep Guardiola alisema haikuwa kazi nyepesi kutwaa ubingwa mbele ya Liverpool aliyodai ilitoa presha kubwa kwao.

Advertisement