Matola kimeeleweka Simba

Monday December 2 2019

 

By Yohana Challe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Uongozi wa Polisi Tanzania umefunguka kuhusu kikao chao na uongozi wa Simba na kwamba umewaruhusu Wekundu wa Msimbazi kumchukua kocha wao Selemani Matola kama ambavyo waliomba.

Mwenyekiti Msaidizi wa Polisi Tanzania, Robert Munisi alisema uongozi wa timu ulipokea barua kutoka Simba ya kumuomba Matola na kwao haikuwa tatizo kwa sababu taratibu zote zilifuatwa.

Alisema mwishoni mwa wiki walikutana na Matola pamoja na uongozi wa Simba na kwa sasa kila kitu kimekwenda safi, kilichobaki Matola kuvunja mkataba kama inavyoelezwa kwenye mkataba wake na wamempa baraka zote za aendako.

“Kwa sasa nipo njiani natoka Dodoma nilipokwenda kukutana na uongozi, hivyo kesho (leo Jumatatu) tutamaliza taratibu zote kuhusu Matola. Timu kwa sasa itakuwa chini ya Ali Suleiman Mtuli ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi hadi pale tutakapokamilisha zoezi la kumpata kocha wa kuziba nafasi hapo baadaye.

“Tunachokingoja ni Matola kuweka mezani fedha za kuvunja mkataba kama tulivyokubaliana wakati tunamchukua kuiongoza timu mwezi Juni mwaka huu, kwa kulipa mara tatu ya mshahara wake aliokuwa akiupokea.

“Siwezi kukuambia kiasi ambacho anatakiwa kukilipa labda yeye akuambie alikuwa analipwa kiasi gani na uzidishe mara tatu, nadhani utakuwa umepata jibu kiasi cha fedha anachotakiwa kukiweka mezani kwa Polisi Tanzania,” alisema Munisi.

Advertisement

Munisi alisema suala hilo limekuwa faraja kwao kwa kuondoka kocha kwa amani bila ugomvi na muda wowote anaweza kurejea maana wamemalizana safi hakuna tatizo lolote ndio maana wamekuwa huru kumwachia na hata wachezaji watakaofuata utaratibu wa kuondoka watawaachia.

Aliongeza kikao walichokaa walijadili mambo kadhaa ikiwamo mwenendo wa timu hiyo kwenye ligi baada ya michezo 11 waliyocheza na kuhusu usajili wa wachezaji kwenye dirisha dogo linalofunguliwa wiki ijayo.

Matola alipoulizwa kuhusu kuacha na Polisi na kurudi Simba timu ambayo aliitumikia kama mchezaji na kisha kuanzia kazi yake ya ukocha, alisema: “Niache kwanza nitakupigia baadaye tuongee vizuri.”

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa Polisi Tanzania, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema baada ya kumalizana na Matola, jina la Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime ndilo linaonekana kuwa mbele kwenda kuziba nafasi hiyo kama mambo yatakwenda vizuri, japo kwa sasa uongozi umeamua kumwachia kazi Mtuli.

“Mtuli ataendelea na kazi kama kawaida ya ukocha huku taratibu nyingine zikiendelea, kuhusu Maxime bado halijakaa sawa japo naliona lipo kwenye mipango hiyo,” kilieleza chanzo hicho.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alipoulizwa kuhusu Matola alisema hizo ni stori tu ambazo hata yeye anazisikia.

Advertisement