Molinga silaha kwa Azam

Dar es Salaam. Yanga wamemrejesha kikosini kinara wao wa mabao waliyetangaza kumtema, David Ndama Molinga, na sasa straika huyo Mkongomani anatarajiwa kubeba silaha za timu hiyo leo wakati itakapowakabili Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayopigwa saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli mapema Alhamisi asubuhi alitangaza orodha ya wachezaji walioachwa katika kikosi hicho na Molinga akiwamo, lakini baada ya muda Ofisa Mhamasishaji Mkuu wa Yanga, Antonio Nuggaz, alitangaza uwepo wa mchezaji huyo kwenye kikosi hicho, kupitia mitandao ya kijamii.

Baada ya mkorogano huo wa taarifa mbili tofauti, Molinga alionekana katika mazoezi ya Yanga iliyokuwa yaliyokuwa yakifanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria, Ubungo wakati ikijiandaa kuivaa Azam.

Mwanaspoti ilimtafuta kocha mpya wa Yanga, Luc Eymael, ambaye alisema wakati anaangalia kanda za video za mechi zilizopita za Yanga aliona moja ya wachezaji ambao wanafanya vizuri kwenye timu hiyo ni straika Molinga, lakini alishangaa kwamba tangu alipotua hakumkuta.

Eymael alisema akawauliza viongozi kuhusu Molinga na alipata majibu kwamba walimuacha mchezaji huyo kutokana na masuala ya kinidhamu ambayo alionyesha, jambo ambalo aliamini si kosa la kuachana na mchezaji huyo na kuomba arudishwe haraka kikosini.

Anasema kikosi cha Yanga licha ya kwamba wamesajili wachezaji watatu katika dirisha dogo ambao ni washambuliaji Ditram Nchimbi, Tariq Seif na Yikpe Gnamein bado hawajafanya vile ambavyo anatamani kuona wanafiti katika mazoezi na mechi ambazo wanacheza chini yake.“Baada ya kuliona hilo nilifikiria haraka Molinga ni mchezaji sahihi ambaye anaweza kuingia katika timu moja kwa moja na akafanya vizuri zaidi ya awali, nikawata viongozi wamrudishe haraka ndani ya timu na nashukuru wameelewa na wamelitimiza hilo,” alisema.

“Molinga kwa aina yake ambavyo anacheza nimemuona anaweza kuongeza kitu katika safu ya ushambuliaji na tukafanya vizuri zaidi kuliko kama angekosekana, lakini nimegundua ni mbunifu wa kupiga mipira iliyokufa ambayo pia ni faida kwetu. “Kuhusu suala la kumtumia katika mechi na Azam litategemea alichofanya katika mazoezi ya siku mbili kabla ya mechi na pia nitashauriana na wasaidizi wangu kisha tutatoka na jibu moja la kumpa nafasi au tumtumie katika mechi zijazo,” alisema.

“Kwa maana hiyo hayo ya nyuma yamepita tunaangalia yajayo,” alisema Eymael ambaye alianza vibaya mechi ya kwanza ya ligi madarakani wakifungwa 3-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru Jumatano.

Molinga ndio kinara wa mabao katika kikosi cha Yanga akiwa amefunga mara nne akilingana na winga Patrick Sibomana.

Rekodi tamu

Katika kipindi cha miaka 10 tangu 2010, Yanga na Azam zimekutana mara 18 na hakuna mbabe kati yao, kila timu imeshinda mara sita na sare ni sita.

Wakati Yanga wanaingia wakitokea kupigwa 3-0 na Kagera Sugar katika mechi ambayo timu hiyo ya Jangwani ilionyesha kiwango kibovu, Azam wana mzuka kama wote baada ya kuifunga Lipuli 2-0 katika mechi yao iliyopita ya Ligi Kuu.

Hata hivyo, rekodi baina ya timu hizo mbili zinampa nafasi yeyote kupata ushindi leo.

Pia mwenendo wa timu hizo kwenye Ligi Kuu Bara unaufanya mchezo baina yao kuwa mkali na wa kuvutia kwani katika mechi tano za ligi za hivi karibuni, Yanga imeshinda mechi mbili, wametoka sare mbili na kupoteza mmoja wakati Azam katika michezo yake mitano ya karibuni, imeshinda mitatu, imetoa sare mchezo mmoja na kupoteza mmoja.

Mtibwa chali

Sherehe za Mtibwa za ubingwa wa Kombe la Mapinduzi zilizimwa jana baada ya kukumbana na kichapo cha 2-0 kutoka kwa KMC katika mechi yao ya Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Uhuru.

Ulikuwa ni ushindi wa kwanza kocha mpya wa timu hiyo Haerman Haruna ambaye amerithi mikoba ya Jackson Mayanja.