Msauzi kuchezesha fainali Senegal v Algeria

Muktasari:

  •  Gomes anakumbukwa na jinsi alivyoacha kilio kwa Ghana baada ya kukataa bao Andre Ayew katika mchezo dhidi ya Tunisia

Cairo, Misri. Mchezo wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon2019) kati ya Algeria na Senegal utachezeshwa na mwamuzi wa Afrika Kusini, Victor Miguel de Freitas Gomes, badala ya Muethiopia Bamlak Tessama Weyesa aliyetangazwa awali.

Hii itakuwa ni mechi ya 52 katika fainali hizi za 32 za Afcon itafanyika kwenye Uwanja wa Cairo International Ijumaa ya Julai 19, 2019.

Mwamuzi Gomes amezaliwa Desemba 15, 1982 katika jiji la Johannesburg.

Amekuwa mwamuzi wa PSL tangu 2008. Gomes alishinda tuzo ya mwamuzi bora wa PSL katika msimu wa 2012–13 na 2017-18 na amekuwa mwamuzi wa kimataifa tangu 2011.

Mwaka 2018, alipewa pongezi na Shirikisho la Soka Afrika Kusini baada ya kukataa kupokea hongo ya kiasi cha Rand 300 000.

Gomes aliwahi kufuata na kuhaidiwa kiasi kikubwa cha fedha ili kupanga matokeo katika mchezo wa Kombe la Shirikisho CAF kati ya timu ya Nigeria ya Plateau United na miamba ya Algeria, USM Alger.

Katika Afcon 2019 nchini Misri, Gomes alichezesha mechi kati ya wenyeji Misri iliyoshinda 2-0 dhidi ya DR Congo.

Pia, alichezesha mechi kati ya Ghana dhidi ya Tunisia katika hatua ya 16 bora.

Katika mechi hiyo, Gomes anakumbukwa na jinsi alivyoacha kilio kwa Ghana baada ya kukataa bao Andre Ayew ambalo lilikuwa goli hali.

Mechi ya mwisho alikuwa mwamuzi wa mezani katika mechi ya nusu fainali kati ya Nigeria na Algeria kwenye Uwanja wa Cairo International.

Algeria ilishinda mechi hiyo kwa mabao 2-1 shukrani kwa bao la dakika za mwisho la nyota wa Manchester City, Riyad Mahrez.

Senegal imefuzu kwa fainali baada ya kuifunga Tunisia 1-0 kwenye Uwanja wa 30th June, mechi iliyoshudia timu zote mbili zikikosa penalti.