Muhuza: Mimi ni Simba damu

MTANGAZAJI maarufu na fundi wa kutangaza mpira wa miguu nchini kutokea katika kituo cha Azam Tv, Baruani Muhuza ameweka wazi kitu ambacho mashabiki walikuwa hawajui. Amefunguka kwamba yeye ni Simba damu lakini hakuwahi kuwabeba popote pale.

Lakini, vilevile amepanga kufungua kituo kikubwa cha soka ambacho kitakuza vijana kutokea mitaani na kuwapeleka timu kubwa nchini na nje ya Tanzania kutokana na mipango ambayo ameiweka.

“Maisha haya ni vyema kujiweka wazi hasa mtu anapofika umri kama wangu inasaidia hata wale waandishi vijana kujifunza vitu. Siwezi kuficha ni kweli mpenzi wa Simba, lakini hakuna mahala nimefanya jambo la kuwasifia au kuwakosoa bila ya sababu ya msingi kwani, kwa muda wote nimekuwa nikifanya kazi yangu kwa uweledi,” anasema.

“Ni vigumu watu kujua mimi ni shabiki wa timu gani, licha ya kutangaza soka kwa miaka 20 japo wachache tu wanajua tena wale niliosoma nao Shule ya Msingi Karuta, Kigoma, Azania hao ndio wanajua.

“Nimefanya kazi nyingi za Yanga ikiwa pamoja na kupanga mikakati ili timu ishinde, nilisafiri nayo kwenda Libya ilipokwenda kucheza na Al-hadad. Kuhusu kujenga kituo cha michezo anasema; “Nimefanikiwa katika kutangaza na eneo kubwa ambalo limenipa nafasi ya kufahamika ni soka hivyo, si muda mrefu nimejipanga kurudisha kwa jamii kile ambacho nimebarikiwa na sababu ya kuamua kufanya jambo hili Ujiji, ambapo nimezaliwa na nimeishi na Mama yangu mzazi ambaye yupo hapo mpaka sasa.”

KASEJA, DIAMOND WAHUSIKA

Muhuza, ambaye matangazo ya mpira ndiyo yamempa umaarufu, anasema katika kuhakikisha anarudisha kwa jamii ameshafanya utaratibu wa kuzungumza na watu mbalimbali ambao wametokea Kigoma ikiwemo kipa wa KMC, Juma Kaseja na msanii wa kizazi kipya Diamond Platinumz.

“Tayari mipango hiyo inakwenda vizuri na kilichobaki ni kuonana na watu hao ili kuzungumza na kufahamu tunaanzia wapi ili kupata eneo ambalo tutalijenga na watu sahihi wa kulisimamia ili kutimiza malengo yetu ya kupata kweli wachezaji vijana na kwenda kuwaendeleza,” anasema.

CHUO CHA UTANGAZAJI

Muhuza anasema kabla ya kupata wazo hilo la kwenda kufungua kituo cha soka Kigoma Ujiji tayari alishaanza mipango ya kufungua Chuo cha Utangazaji atakapostaafu kazi yake pale Azam TV.

“Sina muda mrefu zaidi katika fani hii na nimepanga kurudi nyumbani kwetu Kigoma Ujiji na katika ili niishi kwenye mazingira sahihi muda ambao, nitakuwa huko nitakuwa mwalimu wa utangazaji,” anasema.

“Tayari kuna baadhi ya wadau na mashirika ambao tutakubaliana nao katika hili ili kutoa mchango wao na kwenda kukamilisha uanzishwaji wa chuo ambacho kitatoa watangazaji mashuhuri kwani, mwenyewe ndio nitakuwa nawafundisha,” anasema.

FUNGU LA ASFC

“Kama mambo yapo sawasawa Azam haiwezi kushindwa kulipa timu haki zake kwani, tumeweka Bil 23 kwenye Ligi Kuu kwa miaka mitano ambayo inakaribia kufikia mwisho na hakuna tatizo,” anasema Baruhani ambaye ni miongoni mwa wawakilishi wa Azam kwenye Michuano ya Kombe la FA.

“Inakuwaje mashindano ambayo tunadhamini tuyachezee? Mimi sio msemaji wa hili lakini wanaolalamika lazima waliangalie kwa karibu kwenye hilo.

“Tatizo lilikuwa kwenye mikataba yao, lakini tayari TFF ilikaa na timu na kumaliza mambo yote hivyo huwezi kuja kusikia tena malalamiko.

AUTAKA UBUNGE

Kwa sasa mkongwe huyo anawaza kufikiria namna ya kuachana na kazi ya uandishi wa habari licha ya kuwa kwenye mchakato wa kurudi shule kusomea fani hiyo.

Kwanza kama hujui, Muhuza hana taaluma ya habari, bali kasomea ubaharia pale DMI pamoja Utawala na Uongozi.

“Kwa muda mrefu nimekuwa nikifanya siasa kwa njia ya pembeni kwa maana ya vipindi nilivyokuwa nikiviendesha.

“Nikiwa BBC, Star TV, TBC, na hata hapa Azam nimefanya mahojiano na viongozi wakubwa ndani na nje ya Afrika kama vile Jakaya Kikwete, Joyce Banda, Piere Nkuruzinza, Peter Mutharika na Waziri wa mambo ya nje ya Marekani, Hilary Clinton.

“Kuna vitu vingi natamani kufanya kuihudumia jamii na mwaka huu ndio nataka kugombea ubunge, lakini muda ukifika nitaweka wazi ni wapi nitatangaza nia.

UJUMBE BODI YA LIGI

Muhuza ni miongoni mwa Wajumbe wa Bodi ya Ligi na mapema mwaka huu alitangaza kujiondoa katika nafasi hiyo licha ya kukaa kwa zaidi ya miaka 12, akifanya kazi ya kutoa maamuzi, kusimamia, kuendesha na masuala mengine ya msingi kwenye ligi.

Muhuza anasema si kama aliondoka katika nafasi hiyo ya ujumbe kutokana na malalamiko ya wadau wengi wa soka bali ni majukumu mengi mapya ambayo aliyopangiwa katika ofisi yake ambayo ingemuwia vigumu kushiriki vikao vya bodi kama awali.

“Si kama nimeondoka katika nafasi hiyo ya ujumbe wa bodi kwa sababu ya malalamiko dhidi yetu, hapana bali majukumu mapya ya kazi ambayo nimepangiwa katika kipindi hiki pale ofisini kwangu sitaweza kujigawa katika sehemu mbili,” anasema.

GONDWE, NKAMIA WAMVUTIA

Muhuza anasema anavutiwa na wanahabari wa zamani Juma Nkamia ambaye ni Mbunge wa Chemba Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro kutokana na kazi wanazofanya.

“Nadhani hata mimi siku si nyingi kama nitapata nafasi ya kuingia katika Siasa kama hawa ndugu zangu nitakuwa tayari kwani natamani siku moja nikutane nao tukiwa tunafanya kazi moja kama ilivyokuwa hapo awali,” anasema.