Mwadui: Huyo Bocco, Okwi hawafurukuti!

Wednesday February 14 2018

 

By SADDAM SADICK


Shinyanga. Simba imecheza mechi 17 za Ligi Kuu sawa na dakika 1,530 ikiwa haijapoteza mchezo wowote, ambapo kesho Alhamisi  itakuwa mjini Shinyanga kusaka pointi tatu ili kuendeleza ubabe wake, lakini Kocha  wa Mwadui FC, Ally Bizimungu ameapa kuwatibulia Wekundu hao kwa kuwachapa kwenye mpambano huo.

Mchezo huo ambao utapigwa kwenye uwanja wa CCM Kambarage mjini hapa,unatarajia kuwa mkali na wa kisasi kwani mechi ya awali kwa wapinzani hao, Simba ikiwa uwanja wa Taifa, Dar es Salaam iliwaadhibu Mwadui mabao 3-0.

Kocha Bizimungu alisema kuwa ikiwa ni mara yake ya kwanza kukutana na timu hiyo, anahitaji kuweka rekodi ya kwanza iliyowashinda makocha 15 hadi sasa kwa kuwafunga Simba na kubaki na pointi tatu.

Alisema kuwa licha ya kufahamu kwamba haitakuwa kazi nyepesi, lakini vijana wake wapo fiti na kwamba atamkosa kiungo wake mshambuliaji, Abdalah Seseme aliyeumia enka wakati wa mchezo wao wa kombe la FA dhidi ya Dodoma FC.

“Ni mechi yangu ya kwanza kukutana nao Simba,kwahiyo najua haitakuwa kazi ndogo, lakini nataka nivunje rekodi kwa kuwasimamisha Wekundu hawa yaani hawataamini kitakachotokea”alitamba Mnyarwanda huyo.

Alisema kuwa anaamini kuwa mpambano huo utakuwa mgumu kutokana na kasi ya wapinzani wake waliyoonyesha tangu kuanza kwa Ligi,lakini nia yao ni kuwatuliza leo kwa kichapo.

Alisema kuwa majina anayoyasikia kwenye vyombo vya habari ya Okwi na Bocco kwamba wanatisha, yatapotea  uwanjani kwani silaha alizoandaa ni zaidi ya hao.

“Hayo majina ya Okwi sijui Bocco ni kawaida tu, nataka niwaonyeshe kazi kesho, waliifunga Mwadui kwao, hivyo tunataka kulipa kisasi tukiwa kwetu, kwa hiyo waje tu,” alisema Kocha huyo.

 

Advertisement