KenGold yatangaza vita Ligi Kuu, kikosi kufumuliwa

Mkuu wa wilaya ya Chunya, Mbaraka batunga amesema watashirikiana na uongozi wa KenGold kufanya maandalizi kabambe kwa ajili ya kushiriki Ligi Kuu msimu ujao ambayo yatahusisha usajili wa nyota wapya na kuimarisha benchi la ufundi ili waweze kufanya vizuri.

Batunga ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya timu hiyo kukabidhiwa taji la ubingwa wa Ligi ya NBC Championship baada ya kumalizika kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Pamba iliyoshika nafasi ya pili jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

“Udhamini wa NBC umewezesha kuongeza ushindani kwenye ligi hii na kuboresha soka letu. Leo hii sisi Wanachunya tunajivunia kuwa washindi wa ligi iliyokuwa na ubora kama tulioushuhudia na kupitia ushindani huo tunaamini tunakwenda kutoa changamoto haswa kwenye timu tutakazokutana nazo ligi kuu.  

Baada ya ubingwa huu tunakwenda kujipanga kuanzia kikosi hadi benchi la ufundi ili kujiweka sawa zaidi kwa ajili ya Ligi Kuu, tunawakaribisha sana Chunya,’’ alisema Batunga.

Mkurugenzi wa Biashara wa benki ya NBC, Elvis Ndunguru alisema  itaendelea kuboresha zaidi ligi hizo ili ziendelee kutoa matokeo chanya kulingana na malengo ya udhamini huo.

“Tunawapongeza sana washiriki wote wa ligi ya Championship lakini kiupekee zaidi tunawapongeza Kengold kwa kuibuka washindi kwenye ligi hii. Pongezi zetu pia tunazielekeza Pamba FC kwa kuwa mshindi wa pili na hivyo nae pia anakwenda kushiriki Ligi kuu ya msimu ujao.

 “Pamoja na soka, tumekuwa tukisadia michezo mingine kama gofu na riadha kupitia NBC Dodoma marathon. Nia yetu ya kusaidia sekta ya michezo hapa nchini ni thabiti na tutaendelea kusaidia," alisema Ndunguru.