Yanga Vs Azam, ni fainali ya rekodi, kisasi

Dar es Salaam. Ni rasmi sasa miamba miwili ya soka nchini Yanga na Azam FC zitakutana katika fainali ya Kombe la CRDB (CBFC), ambayo inatarajiwa kuchezwa Juni 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Tanzanite, uliopo mjini Babati mkoani Manyara.

Azam ilifuzu hatua hiyo baada ya ushindi mnono wa mabao 3-0, dhidi ya Coastal Union yaliyofungwa na nyota wa kikosi hicho, Abdul Suleiman 'Sopu' aliyefunga mawili na Feisal Salum 'Fei Toto', mechi ikipigwa Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

Huku Yanga yenyewe ikifika hapa baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ihefu kwenye mchezo mkali uliopigwa kwa dakika 120 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.

Wakati miamba hiyo ikikutana katika mchezo huo utakaovuta hisia za mashabiki, kila mmoja amekuwa akiamini kuwa hii ni fainali ambayo haina mwenyewe kutokana na ubora wa timu zote mbili msimu huu.


Mechi ya kisasi

Mchezo huu utakuwa ni fainali ya nne kwa Azam FC tangu michuano hii iliporejea rasmi mwaka 2015 na kati ya hizo mara mbili ilipokutana na Yanga na haikuweza kufua dafu kwa sababu ilishindwa kutamba na kujikuta ikichezea vichapo zote.

Fainali ya kwanza kwa timu hizo kukutana ilipigwa Mei 25, 2016, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo Azam FC ilifungwa mabao 3-1, mabao ya Amissi Tambwe aliyefunga mawili na Deus Kaseke huku lao la kufutia machozi likifungwa na Didier Kavumbagu.

Kama haitoshi msimu uliopita zikakutana tena katika fainali ya michuano hii iliyopigwa Juni 12, kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ambapo Azam FC ikachezea tena kichapo cha bao 1-0, lililofungwa na Mzambia, Kennedy Musonda.

Sopu anaisubiri Yanga

Abdul Suleiman 'Sopu' wa Azam FC ndiye anayeshikilia rekodi ya mchezaji aliyefunga mabao matatu yaani 'hat-trick' katika mchezo wa fainali ya michuano hii aliyoiweka msimu wa 2021-2022, wakati huo akiichezea Coastal Union maarufu 'Wagosi wa Kaya'.

Sopu aliweka rekodi hiyo wakati wa mchezo wa fainali iliyopigwa Julai 2, 2022 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ambapo Coastal Union ilitoka sare ya mabao 3-3, dhidi ya Yanga kisha kukosa ubingwa kwa kufungwa kwa penalti 4-1.

Mabao ya Yanga kwenye mchezo huo yalifungwa na Feisal Salum 'Fei Toto' dakika ya 57, Heritier Makambo dakika 82 na Denis Nkane dakika ya 113 huku yale yote ya Coastal Union yakifungwa na 'Sopu' katika dakika ya 11, 88 na 98.

Katika penalti nne za Yanga walizopata zilifungwa na Yannick Bangala, Heritier Makambo, Dickson Job na Khalid Aucho huku Coastal Union wakipoteza mbili na kufunga moja iliyofungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho Mnigeria, Victor Akpan.


Yanga rekodi

Tangu michuano hii iliporejea mwaka 2015, Yanga imeingia fainali nyingi zaidi tofauti na timu yoyote ikifanya hivyo mara tano.

Mara nne iliyoingia ni fainali moja tu ambayo haikuchukua ubingwa ambao ni msimu wa 2020-2021, iliponyukwa na watani zao wa jadi Simba bao 1-0, lililofungwa na Taddeo Lwanga, mechi ikipigwa Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma Julai 25, 2021.

Tangu kuanza kwa michuano hii mwaka 1967 ikifahamika kwa jina la FAT kabla ya 2015 kubadilishwa na kuitwa ASFC, Yanga ndio timu iliyotwaa mara nyingi ubingwa ikifanya hivyo mara saba kuanzia 1967, 1974, 1998, 2001, 2015-2016, 2021-2022 na 2022-2023.

Timu inayofuatia ni watani zao Simba ambao imechukua taji hili mara nne ikianzia, 1995, 2016-2017, 2019-2020 na 2020-2021.

Azam inasaka la pili:

Hii ni fainali ya nne kwa Azam FC katika mashindano haya ambapo mara tatu ilizotinga imelichukua mara moja tu ikifanya hivyo msimu wa 2018-2019, ilipoifunga Lipuli ya mkoani Iringa bao 1-0, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ilulu Lindi.

Mchezo huo uliopigwa Juni Mosi, 2019, bao pekee la Azam lilifungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo Mzambia, Obrey Chirwa dakika ya 64.