Mwadui kumenuka unaambiwa, wachezaji watishia kugoma

Muktasari:

  • Mwadui imekuwa na mwenendo mbaya hali iliyoanza kuzua taharuki kwa mashabiki wa timu hiyo.

HUKO mgodini katika klabu ya Mwadui FC hali si shwari baada ya wachezaji kudai mishahara  yao takribani miezi mitatu huku kukiwa hakuna hata dalili ya kulipwa mishahara yao.

Mwadui ambayo inashikilia nafasi 19 (Pili kutoka chini) ikiwa na pointi 37 katika michezo 35 imezidi kuwa katika hali tete baada ya kutoka sare ya 3-3 dhidi ya Mbao katika Uwanja wa Mwadui Complex.

Mmoja wa wachezaji alilidokezea Mwanaspoti kwamba hawajapokea mishahara yao huku viongozi wakiwa wameitelekeza timu kutokana na kuwa katika sintofahamu na benchi la ufundi.

“Kaka nakuambia ukweli hapa hakuna aliyepata mishahara hata ela ya vocha wengine wanakosa, lakini wachezaji wamekuwa wakijituma muda wote wanapokuwa uwanjani, watupe hata mashahara wa mwezi mmoja” alisema.

Aliongeza kwamba licha ya viongozi hao kuambiwa bado walikuwa kimya katika kutoa maamuzi ya mwisho kutokana kuwa na mgogoro wa chinichini na  benchi la ufundi.

Hata hivyo Mwanaspoti lilimpigia Katibu mkuu wa timu hiyo, Ramadhan Kilao ili aweze kutolea ufafanuzi alisema” Kuhusu hilo suala nipigie baadaye hivi sasa naingia msikitini,” alisema hivyo jana jioni (Alhamis).

Mwananchi lilisubili mpaka baada ya swala ya jioni na kuendelea kumpigia hata hivyo Katibu huyo hakupokea simu mpaka gazeti linaingia mtamboni.

Chanzo kingine kililidokeza Mwanaspoti kwamba tofauti za Uongozi na benchi la ufundi zilianza baada ya kocha huyo kupeleka barua ya malimbikizo ya mishahara na pesa zake za usajili Tff.