Nyota Stars wapania kumtibulia kipa Uganda

Muktasari:

  • Wachezaji wengine kama Shaaban Iddi Chilunda na Farid Mussa, wanaoicheza soka la kulipwa nchini Hispania pamoja na Yahaya Zayd anayeichezea Ismailia ya Misri ni miongoni mwa washambuliaji wazuri wanapokuwa uwanjani na wanaweza kutibua rekodi ya kipa Onyango.

Dar es Salaam. Shughuli ipo kesho pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Taifa Stars itakapovaana na Uganda.

Mbali ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika, ushindi wa Taifa Stars utakuwa pigo kwa kipa wa Uganda, Dennis Onyango ambaye pia ni nahodha wa timu hiyo.

Kipigo chochote ambacho Stars itakitoa kwa Uganda kwenye mechi hiyo, kitamaanisha kuvunjika kwa rekodi ya kutoruhusu bao ambayo Onyango amekuwa nayo katika mashindano hayo ya kuwania kufuzu Afcon awamu hii.

Katika mechi tano ambazo Uganda imecheza hadi sasa, Onyango hajaruhusu nyavu zake kutikiswa hata mara moja huku akiwa amecheza mechi hizo zote lakini kiu ya nyota wa Stars kusaka ushindi kwenye mchezo wa kesho inaweza kumfanya ajikute kwenye wakati mgumu.

Mechi hizo tano ambazo OnMechi hizo tano ambazo Onyango hajaruhusu nyavu ni ile ya ushindi wa bao 1-0 nyumbani na ugenini dhidi ya Cape Verde, walipoifunga Lesotho mabao 3-0 nyumbani kisha 2-0 ugenini na ile dhidi ya Taifa Stars waliotoka sare ya bila kufungana.yango hajaruhusu nyavu ni ile ya ushindi wa bao 1-0 nyumbani na ugenini dhidi ya Cape Verde, walipoifunga Lesotho mabao 3-0 nyumbani kisha 2-0 ugenini na ile dhidi ya Taifa Stars waliotoka sare ya bila kufungana.

Lakini Onyango huenda safari hii akakutana na kibarua kizito mbele ya nyota wa Stars hasa Samatta kutokana na viwango bora ambavyo wamekuwa wakionyesha kwenye klabu zao katika siku za hivi karibuni.

Ukianzia kwa Samatta, nahodha huyo wa Stars kwa sasa ndiye kinara wa ufungaji kwenye Ligi Kuu ya Ubelgiji akiwa amepachika mabao 20 katika mechi 28 alizocheza lakini kiujumla amefumania nyavu mara 29 katika michezo 41 ya mashindano tofauti wanayoshiriki.

Lakini pembezoni mwa Samatta atakuwapo Saimon Msuva ambaye amekuwa tishio kwenye Ligi Kuu ya Morocco msimu huu akiwa hadi sasa ameifungia timu yake ya Difaa El Jadida mabao nane katika mechi 15 alizoichezea. Mbali na Samatta na Msuva, Onyango pia anapaswa kujiandaa kukabiliana na Thomas Ulimwengu ambaye anaonekana ameanza kuimarika hivi sasa tofauti na miezi kadhaa iliyopita kutokana na kuanza kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu yake ya JS Saoura ambacho amekifungia bao moja katika mechi 11 alizokichezea za mashindano mbalimbali.

Mchezaji mwingine anayeweza kuharibu rekodi ya Onyango Jumapili ni John Bocco ‘Adebayor’. Bocco ameifungia Simba mabao tisa kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu na yuko moto kweli kweli hivi sasa hivyo anaweza akawa chachu ya ushindi wa Taifa Stars siku hiyo kama atacheza katika ubora wake.

Pia Shiza Kichuya anayeichezea klabu ya ENPPI ya Misri licha ya kwamba hajaifungia bao lolote timu yake katika Ligi Kuu nchini humo lakini ni mmoja ya mawinga hatari hapa nchini na wakati wowote anaweza kuamua mechi.

Wachezaji wengine kama Shaaban Iddi Chilunda na Farid Mussa, wanaoicheza soka la kulipwa nchini Hispania pamoja na Yahaya Zayd anayeichezea Ismailia ya Misri ni miongoni mwa washambuliaji wazuri wanapokuwa uwanjani na wanaweza kutibua rekodi ya kipa Onyango.

Nyota wengine wanaotishia ‘kumwagia mchanga pilau’ la rekodi ya kipa huyo ni mabeki na viungo ambao pia ni wanalijua goli kama Himid Mao ambaye ameifungia timu yake ya Petrojet ya Misri mabao mawili mpaka sasa hivyo anaweza kuibeba pia Taifa Stars sambamba kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ mwenye mabao matatu kwenye ligi.