Pepe shakani, Aguero nje Arsenal v Man City

London, England. Mshambuliaji wa Arsenal, Nicolas Pepe ataangaliwa kwa mara ya mwisho goti lake kabla ya mechi yao ya leo ya Ligi Kuu England watakayowakaribisha Manchester City kwenye Uwanja wa Emirates.

Mchezaji huyo aliyesajiliwa kwa dau lililoweka rekodi ya uhamisho ya klabu hiyo alikosa mechi yao ya Ligi ya Europa ugenini dhidi ya Standard Liege Alhamisi iliyomalizika kwa sare ya 2-2 kutokana michubuko katika goti lake lakini anapewa nafasi ya kuwavaa mabingwa watetezi leo.

Hector Bellerin (misuli ya nyuma ya paja) pia ataangaliwa hali yake kama ataweza kucheza lakini Kieran Tierney (bega), Granit Xhaka (aliyegongwa kichwani), Rob Holding (goti) na Danny Ceballos (misuli ya nyuma ya paja) wote watakosa mechi ya leo.

Arsenal wamepoteza mechi zao zote nne za ligi walizokutana na Manchester City. Mara ya mwisho kupoteza mechi tano mfululizo katika ligi ilikuwa ni dhidi ya Manchester United kati ya Septemba 1983 na Agosti 1985.

Manchester City wameshinda mechi zote mbili zilizopita za Ligi Kuu ugenini Emirates dhidi ya Arsenal – idadi ambayo ni kubwa kuliko walichovuna katika mechi 32 zilizotangulia walizoenda Highbury/Emirates ambapo walishinda mechi moja sare 11 na vipigo 20 (W1 D11 L20).

Mechi nyingine zitakazopigwa leo ni Manchester United yenye mzuka mpya ambayo itaivaa Everton iliyotokea kuichakaza Chelsea 3-1, huku pia Wolves ikiikaribisha Tottenham.