Prime
Waarabu sasa wamtaka beki Simba

Muktasari:
- Simba imepokea ofa kutoka Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na RS Berkane Morocco zote zikionyesha nia ya kunasa saini ya mshambuliaji huyo raia wa Uganda.
Licha ya Simba kushindwa kufikia malengo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa nne mfululizo timu mbalimbali zinaendelea kupishana kuwania saini za baadhi ya nyota baada ya USM Alger ya Algeria kutuma ofa ya kumhitaji beki wa kati Che Malone Fondoh, huku mastaa watatu wakiwa wameshaaga.
Che Malone, alitua Msimbazi misimu miwili iliyopita akitokea Coton Sport ya Cameroon na kutengeneza ukuta mgumu sambamba na Henock Inonga aliyetimka klabuni hapo na sasa akishirikiana na Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue ukuta ambao umeifanya Simba kuendelea kuwa imara na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.
Beki huyo wa kati licha ya kutokuwa na msimu mzuri kama ilivyokuwa msimu wake wa kwanza alipojiunga na timu hiyo kutokana na kusumbuliwa na majeraha ameingia kwenye rada za timu kubwa Afrika ya USM Alger ambayo imemaliza msimu wa Algeria ikiwa nafasi ya nane kwenye msimamo.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba kinasema kuwa uongozi wa timu hiyo ulipokea ofa kuhusu beki huyo raia wa Cameroon ambayo ina dau la kuridhisha na klabu hiyo haiwezi kuikataa.
Hata hivyo Mwananchi linafahamu kuwa uongozi wa Simba na benchi la ufundi halikuwa na mpango wa kuendelea na beki huyo kwa ajili ya msimu ujao akiwa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja.
"Ni kweli kuna ofa nyingi mezani kwetu kuwahitaji wachezaji, siwezi kuzungumzia mchezaji mmoja ambaye pia sina taarifa zake ninachoweza kukuthibitishia ni kwamba msimu huu tutafanya biashara na tutasajili wachezaji wazuri zaidi ya wale ambao wanaondoka.
"Ishu Che Malone nami naisikia, lakini sitaki kukuthibitishia kama ipo au haipo jambo la kusubiri ni kuona aina ya usajili ambao tutaufanya kabla dirisha halijafungwa na wachezaji ambao wataondoka, lakini nafikiri hata timu itafurahi kupata ofa hiyo."
Mtoa taarifa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, amesema timu yao ilikuwa na kikosi kizuri pamoja na kushindwa kufikia malengo na ndio maana ofa zimekuwa nyingi na wao hawana sababu ya kuendelea kuwang'ang'ania wachezaji wao.
Ukiachana na Che Malone, Mwananchi linafahamu kuwa Simba pia ipo kwenye hatua nzuri ya kumuuza mshambuliaji wake Steven Mukwala ambaye amemaliza msimu vizuri akifunga mabao 13 kwenye Ligi Kuu Bara.
Simba imepokea ofa kutoka Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na RS Berkane Morocco zote zikionyesha nia ya kunasa saini ya mshambuliaji huyo raia wa Uganda.
Endapo mastaa hao wakiondoka, Simba itakuwa imeshaachana na wachezaji watano baada ya Hussein Kazi, Fabrice Ngoma ambao mikataba yao imemalizika na tayari wameshaanga pamoja na beki wa pembeni Valentin Nouma ambaye amefikia makubaliano na timu hiyo kutokana na kukosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mara kwa mara, akiwa ametoa pasi mbili tu za mabao msimu huu.
Akizungumza jana, Mkuu wa Idara ya Habari wa Simba Ahmed Ally, alisema ni kweli wamefikia makubaliano ya kuachana na beki na baadhi ya wachezaji lakini watarudi sokoni na kutafuta wachezaji bora zaidi ya hao wanaoondoka.
"Kuna wachezaji tutaachana nao, na wengine watabaki, lakini kama klabu kwa sasa tunachotaka kufanya ni kuhakikisha mchezaji anayesajiliwa anakuwa na kiwango cha juu, yaani kusiwe na tofauti ya yule anayeanza na anayeingia.
"Kwa upande wa Nouma, tunaheshimu uwezo wake, lakini hakufikia malengo ya Simba ndiyo maana ameondoka kwenye kutafuta changamoto sehemu nyingine, kila kinachofanyika kwa sasa kina baraka zote za kocha mkuu Fadlu Davids," alisema Ahmed.